1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Belarus zafanya pamoja mazoezi ya kijeshi

Angela Mdungu
10 Septemba 2021

Mataifa 10 yanashiriki katika mazoezi ya kijeshi ya kimkakati leo Septemba 10 katika vituo vinne vya mafunzo huko Belarus na vinane nchini Urusi. Mataifa jirani zimetangaza pia kuwa na mazoezi ya aina hiyo

https://p.dw.com/p/409l8
Russland Präsident Putin trifft Alexander Lukaschenko in Moskau
Picha: Mikhail Voskresensky/Sputnik/AP Photo/picture alliance

Nchi nyingine jirani zimetangaza pia kuwa na mazoezi ya aina hiyo. Mazoezi hayo ya kijeshi ni hatua ya mwisho ya mazoezi ya pamoja ya wanajeshi wa Belarus na Urusi kwa mwaka huu.

Katika mazoezi hayo ya kijeshi yanayojulikana kama Zapad 2021, jumla ya wanajeshi 200,000 wanatarajiwa kushiriki. Kwa mujibu wa taarifa kutoka Belarus ni wanajeshi 12,800 pekee wakiwemo 2,500 kutoka Urusi na 50 wa Kazakhstan, ndiyo watakaohusishwa katika ngwe ya kwanza inayoanza Belarus. Ndege za kijeshi 80, helikopta na karibu vifaa vya kijeshi 760, yakiwemo matanki 290, bunduki 240, roketi kadhaa Pamoja na meli 15 zitahusika kwenye mazoezi hayo.

Hadi sasa vikosi vya Jumuiya ya mkataba wa usalama wa pamoja (CSTO) vimekuwa vikifanya mazoezi ya kijeshi Urusi na Belarus kila baada ya miaka miwili. Kwa mara ya mwisho, mazoezi hayo yalifanyika mwaka 2017. 

Mataifa mengi zaidi katika awamu ya pili 

Mwaka huu, wanajeshi kutoka Armenia, Kazakhstan, India, Kirgisztan, Mongolia, Serbia na Sri Lanka nao watashiriki katika sehemu ya pili ya mazoezi hayo yatakayofanyika kwenye ardhi ya Urusi. Nchi za China, Vietnam, Myanmar, Pakistan na Uzbekistan zitatuma waangalizi. 

Weißrussland Zapad-2017 Militärmanöver
Roketi ikirushwa katika mazoezi ya kijeshi ya Zapad, 2017.Picha: Reuters/Vayar military information agency/Belarussian Defence Ministry

Akizungumzia mazoezi hayo ya kijeshi, Sarhei Bohdan wa wa taasisi ya Historia ya chuo kikuu Free University cha mjini Berlin anasema awali Belarus ilikuwa na ushawishi mkubwa lakini sasa yamekuwa kama maonesho ya kijeshi ya Urusi. Ameongeza kuwa hata hivyo, kitendo cha jeshi la Kazakhstan na nchi nyingine kushiriki katika mazoezi hayo ni mafanikio. 

Mazoezi ya  "Zapad 2021" yanafanyika ili kujiweka tayari kwa migogoro na mizozo inayohusishwa na ongezeko la makundi ya wabeba silaha ambayo ni kinyume cha sheria, watu wanaotaka kujitenga na makundi ya kimataifa ya kigaidi.

Katika mazoezi ya kijeshi ya mwaka 2017, waangalizi wa Ulaya walihofia kuwa baadhi ya wanajeshi wa Urusi wangesalia Belarus. Na sababu ya hofu hiyo inatajwa kuwa ni mahusiano yaliyojaa mivutano kati ya Urusi na Ukraine. Kumekuwa na hisia kama hizo mwaka huu huku baadhi ya watu wakiituhumu Urusi na Belarus kuwa zinaandaa vita inayohusisha operesheni za kivita, mashambulizi ya mtandao na propaganda dhidi ya Umoja wa Ulaya.