Upinzani Tanzania wakaidi agizo la msajili wa vyama | Matukio ya Afrika | DW | 18.07.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Upinzani Tanzania wakaidi agizo la msajili wa vyama

Vyama vya upinzani nchini Tanzania vimesema havitaheshimu agizo la msajili wa vyama vya siasa nchini humo la kuvitaka kufungua ofisi jijini Dodoma.

Vyama vya upinzani nchini Tanzania vimesema havitazingatia ushauri wa msajili wa vyama vya siasa aliyeviandikia kutaka vifungue ofisi Dodoma ambako yeye mwenyewe anakusudia kuhamishia ofisi yake. Vyama hivyo vimesema siyo kwamba ushauri huo hautekelezeki kwa mantiki za kiuchumi lakini pia unakwenda kinyume na katiba zao. 

Vyama hivyo vinasema suala la wapi yawe makao makuu ya chama ni jambo la kimkakati na kwa maana hiyo havikubaliani na barua iliyoandikwa na msajili huyo akivishauri vihamie huko Dodoma ambako pia serikali imehamishia makao yake makuu.

Barua ya msajili kwenda kwa vyama hivyo imesema kuwa ofisi yake inapanga kuhamishia makao yake Dodoma na kwa jinsi hiyo hakutakuwa na huduma zozote kutoka Dar es salaama na akavishauri vyama navyo kwenda Dodoma.

Akizungumzia kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi wa itifaki na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema amesema kwenda Dodoma haitawezekana kwa chama hicho.

Mbali ya kwamba suala la kuhamia Dodoma ni lenye gharama lakini pia amedai jambo hilo halitekelezeki kwa vile ni kinyume na katiba ya chama.

Upinzani Tanzania umesema ushauri wa msajili wa vyama vya siasa unaenda kinyume na katiba zao

Upinzani Tanzania umesema ushauri wa msajili wa vyama vya siasa unaenda kinyume na katiba zao

Nacho chama cha ACT Wazalendo ambacho hivi karibuni kilipata nguvu mpya za kisiasa baada ya kuwapokea vigogo waliojiengua kutoka Cuf, kimepinga wazo la kwenda Dodoma.

Mkuu wa Itikadi na uenezi Ado Shaibu amesema siasa ni mchezo wa kimkakati unaofanywa kulingana na utashi na matakwa ya chama na kwa maana hiyo suala la wapi yawe makao makuu ya chama haliwezi kuamuliwa na taasisi nyingine.

Kumekuwa na madai kuwa suala la kuhamia Dodoma limekuwa likigharimu kiasi kikubwa cha fedha. Wataalamu wa masuala ya ujenzi wanasema kwamba ujenzi wa ofisi moja ya watu 100 unaweza kugharimia mamilioni ya fedha.

Tangu utawala wa awamu ya tano uingie madarakani umekuwa ukizihamishia taasisi na ofisi zake mjini Dodoma ambako pia chama tawala CCM ni chama pekee cha siasa chenye makao yake makuu huko.