Upinzani Syria kushiriki mazungumzo ya amani | Matukio ya Kisiasa | DW | 11.11.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Upinzani Syria kushiriki mazungumzo ya amani

Kundi kubwa la upinzani nchini Syria linaloungwa mkono na mataifa ya Magharibi, limesema linakusudia kushiriki katika mazungumzo ya amani na serikali ya Syria yatakayofanyika Geneva, iwapo matakwa yao yatatimizwa.

Wajumbe wa muungano wa upinzani wa Syria, mjini Istanbul

Wajumbe wa muungano wa upinzani wa Syria, mjini Istanbul

Baada ya kura iliyopigwa mapema leo asubuhi mjini Istanbul, Muungano wa Upinzani wa Syria-SNC, umewaruhusu wawakilishi wake kuhudhuria mkutano wa amani kati yake na serikali ya Rais Bashar al-Assad. Marekani na Urusi zinajaribu kuendeleza juhudi za kuanzisha mazungumzo ya Geneva ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Lakini kwa mujibu wa taarifa ya muungano huo wa upinzani, wawakilishi wake watahudhuria mkutano huo wa kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe, kwa masharti kwamba serikali ya Syria iruhusu mashirika ya misaada kuyafikia maeneo yaliyoathiriwa na mizozo na kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa na watu wengine wanaowashikilia hasa wanawake na watoto.

Ahmad al-Jarba, kiongozi wa muungano wa upinzani wa Syria

Ahmad al-Jarba, kiongozi wa muungano wa upinzani wa Syria

Aidha upinzani huo unataka mazungumzo yoyote yale ya kisiasa yawe matokeo ya kuwepo kwa muda wa mpito wa kisiasa. Taarifa hiyo imetolewa na ofisi ya Monzer Azbik, kiongozi mkuu wa wafanyakazi kwa mwenyekiti wa muungano wa kitaifa, Ahmad al-Jarba, baada ya kura kupigwa leo katika siku ya pili ya mikutano inayoendelea mjini Istanbul.

Taarifa hiyo imeweka wazi kwamba uamuzi huo haujaondoa madai yao ya kutaka Rais Assad aondoke madarakani katika serikali yoyote ile ya mpito.

Assad kutokuwa na jukumu lolote lile

Taarifa hiyo imesema kuwa Rais Assad hatokuwa na jukumu katika kipindi cha mpito na serikali ya baadaye ya Syria. Muungano huo wa upinzani pia unatarajiwa kuidhinisha orodha ya majina ya mawaziri wake, yaliyowasilishwa na waziri mkuu wa mpito aliyechaguliwa na upinzani mwezi Septemba, Ahmad Toumeh.

Wanaharakati wanasema kuwa uamuzi huo unafuatia makubaliano yaliyofikiwa jana Jumapili (10.11.2013), kupunguza kizuizi kilichokuwa kimewekwa kwenye mji wa waasi karibu na mji mkuu wa Damascus, kwa kuruhusu chakula kuwafikia raia kwa mara ya kwanza katika kipindi cha wiki kadhaa.

Rais wa Syria, Bashar al-Assad

Rais wa Syria, Bashar al-Assad

Kundi la wanaharakati na waandishi wa habari wa mji huo wa Qudsaya, limethibitisha kuhusu makubaliano hayo, na mwanzoni mwa mwezi huu lilisema kuwa masoko yameishiwa vyakula na wananchi masikini katika eneo hilo wanakabiliwa na uhaba wa chakula.

Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binaadamu la Syria, Rami Abdel Rahman, amesema makubaliano hayo yaliruhusu chakula na unga kupelekwa kwenye mji huo.

Katika wiki za hivi karibuni, wapatanishi kadhaa wa mzozo wa Syria, wamekuwa wakijaribu kupunguza vikwazo vilivyowekwa kwenye maeneo kadhaa. Serikali ya Syria inakabiliwa na shinikizo la kimataifa kuruhusu msaada wa chakula na dawa, kuyafikia maeneo yenye vizuizi.

Wakati huo huo, mapigano ya kugombania udhibiti wa ngome muhimu inayoulinda uwanja wa ndege ambao unadhibitiwa na serikali kaskazini mwa mji wa Aleppo, bado yanaendelea.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE
Mhariri: Gakuba Daniel

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com