1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi zaendelea kuufanikisha mkutano wa Syria

5 Novemba 2013

Urusi, Marekani na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Lakhdar Brahimi, kwa kauli moja wamekubali kutuma ujumbe kwa wahusika katika mazungumzo ya kuisaka amani ya Syria.

https://p.dw.com/p/1ABt5
Mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Lakhdar Brahimi
Mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Lakhdar BrahimiPicha: Reuters/Khaled al-Hariri

Hii ni kulingana na duru ndani ya vikao vya kupanga mazungumzo hayo zilizolifikia shirikia la habari la dpa. Amina Abubakar na habari hiyo. Duru hizo hata hivyo hazikueleza siku rasmi ya kufanyika mazungumzo ya amani ya Syria, huku shirika la habari la Urusi, Itar-Tass, likisema kuwa mazungumzo hayo hayatafanyika tena mwezi huu. Awali mazungumzo hayo yalitarajiwa kuanza tarehe 23 mwezi huu kama ilivyopendekezwa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu.

Shirika hilo la habari la Urusi limeripoti kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amepanga kutuma ujumbe wa mualiko wa mazungumzo hayo ambayo kwa sasa hayajulikani yataanza lini kwa serikali ya Syria, upinzani na nchi nyengine zinazoathirika kufuatia mapigano yaliodumu kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

Hii leo Brahimi ameendelea kukutana na maafisa wa Marekani na Urusi kuzungumza namna na kufanikisha mazungumzo hayo huku kukiwa na masuala tete ya mustakbal wa Rais Bashar al-Assad na iwapo mshirika wake Iran anaweza kuhudhuria mazungumzo hayo ya amani. Urusi imesisitita Iran ni lazima ihudhurie mazungumzo hayo hasaa baada ya baada ya kiongozi wa upinzani Ahmed Jarba kusema muungano wake hautahudhuria kikao hicho iwapo Iran itakuwa ndani ya mazungumzo hayo.

Awali serikali ya Syria kupitia waziri wa habari Omran Zoabi ilisema Assad atabakia madarakani na kutishia kutohudhuria mazungumzo hayo iwapo Rais Assad atatakiwa kuondoka uongozini. Omran Zoabi amesema Syria, itabakia kama taifa pamoja na majimbo yake yote na watu wake pia na rais Assad ataendelea kuwa rais wa nchi hiyo hata kama wengine wanandoto ya kuwa Assad ataondoka madarakani.

Idadi ya wakimbizi inaendelea kuongezeka nchini Syria kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe
Idadi ya wakimbizi inaendelea kuongezeka nchini Syria kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewePicha: Reuters

Hatua hii imetoa shaka ya kuwa na serikali ya mpito jambo linalotarajiwa kuhimizwa katika mkutano huo unaojulikana kama Geneva 2. Baadaye Brahimi anatarajiwa kuwa na mkutano na nchi nyengine tatu wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ambayo ni Uingereza, Ufaransa na Uchina, pamoja na majirani wa Syria, Iraq Jordan, Lebanon, Uturuki na pia Jumuiya ya nchi za kiarabu.

Juhudi za kimataifa za kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria vilivyosababisha mauaji ya zaidi ya watu 100,000 na kusababisha mamilioni kukimbia makaazi yao zinaonekana kukumbwa na changamoto kuu. Wakati huo huo waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry amesema jambo la hakika kwa hivi sasa ni kwamba Syria haitoingiliwa kijeshi lakini akasisitiza ni lazima Assad an'gatuke madarakani.

Huku hayo yakiarifiwa mfalme wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani, amedai kuwa mapendelezo yaliotolewa ili kufanyika kwa mazungumzo ya amani hayana msingi akisema mazungumzo hayatafua dafu na kwamba mazungumzo hayo yanapaswa kuto haki kwa raia wa Syria.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/Reuters/AP

Mhariri: Mohammed Khelef