Unyanyasaji wa kingono Ufaransa aibu kwa kanisa asema Papa | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.10.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Unyanyasaji wa kingono Ufaransa aibu kwa kanisa asema Papa

Papa Francis ameelezea aibu iliyolikumba kanisa pamoja na yeye mwenyewe kutokana na kiwango cha unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto uliofanywa na kanisa nchini Ufaransa.

Matamshi hayo ameyatoa leo mjini Vatican katika mahubiri yake ya kila Jumatano kwa waumini ambapo amezungumzia takriban watoto 330,000 wa Ufaransa ambao walinyanyaswa na mapadri na viongozi wengine wa kanisa hilo kuanzia miaka ya 1950. Amesema idadi hiyo ni kubwa na kwamba anasikitishwa  na mateso ya kiwewe kwa wahanga wa unyanyasaji huo.

''Ningependa kuwaelezea wahanga huzuni yangu na maumivu yangu kutokana na kiwewe walichopata na aibu yangu, aibu yetu.  Aibu yangu kwa kutoweza kwa kanisa kwa muda mrefu sana kuyashughulikia ipasavyo madhila ya waathirika, kwa kuwahakikishia maombi yangu. Ninaomba na tuombe wote pamoja : kwako, Bwana, utukufu, kwetu aibu. Huu ni wakati wa aibu.'',alisema Papa Francis.

Papa Francis amewataka maaskofu wote na viongozi wa kidini kuchukua hatua zote muhimu ili vitendo kama hivyo visijirudie tena. Aidha, papa pia amewataka Wakatoliki wa Ufaransa kuhakikisha kwamba kanisa linabaki kuwa nyumba salama kwa wote.

Soma pia: Papa asema dini isitumiwe kwa malengo ya kisiasa

Unyanyasaji kwa njia ya kimfumo

Ripoti hiyo ilisema makasisi wanaokadiriwa kuwa 3,000 na idadi isiyojulikana ya watu wengine wanaohusishwa na Kanisa Katoliki waliwanyanyasa kingono watoto. Kanisa la Ufaransa, kama ilivyo katika nchi zingine, limelazimika kukabiliana na kashfa hizo ambazo zilifunikwa kwa muda mrefu.

Mwenyekiti wa tume huru iliyotoa matokeo, Jean-Marc Sauve, alisisitiza Jumanne kuwa viongozi wa Kanisa kwa miaka 70 walikuwa wameficha unyanyasaji huo kwa njia ya kimfumo.

Soma pia :Papa Francis awahimiza Wakristo kutopoteza tumaini

Kanisa kuchangia fidia kwa waathiriwa 

Waathiriwa wa visa vya unyanyasaji kingono nchini Ufaransa wapongeza ripoti

Waathiriwa wa visa vya unyanyasaji kingono nchini Ufaransa wapongeza ripoti

Waathiriwa walipongeza ripoti hiyo ya kurasa 2,500 licha ya kwamba imechelewa, na mkuu wa kongamano la maaskofu wa Kanisa Katoliki wa Ufaransa aliwaomba msamaha.

Tume huru ya uchunguzi ilihimiza kanisa kuchukua hatua kali, kukemea makosa na kimya chake. Iliitolea pia wito Kanisa Katoliki kusaidia kulipa fidia waathiriwa, haswa katika kesi ambazo ni za zamani kushtakiwa katika korti za Ufaransa.

Papa Francis alipitisha sheria kuu ya kanisa mnamo Mei 2019, inayohitaji mapadri na watawa wote wa Katoliki kuripoti unyanyasaji wa kijinsia wa makasisi na wakubwa wao kwa viongozi wa kanisa. Mwezi Juni Francis alisema kwamba kila askofu lazima achukue jukumu la "janga" la tatizo la unyanyasaji wa kijinsia.