1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNHCR: Wanaowakataa wakimbizi wa Syria ni washirika wa IS

Caro Robi22 Desemba 2015

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia wakimbizi UNHCR amesema watu wanaowakataa wakimbizi wa kutoka Syria nchini mwao ndiyo washirika wakubwa wa wanamgambo wenye itikadi kali wa Dola la Kiislamu IS.

https://p.dw.com/p/1HRVo
Picha: picture-alliance/dpa/J.-Ch. Bott

Antonio Guterres ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo jana kuwa takriban wakimbizi milioni 4.3 wanaovitoroka vita vya karibu miaka mitano Syria hawawezi kulaumiwa kwa ugaidi wanaohatarisha maisha yao kuukimbia.

Akimshutumu mgombea Urais wa chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump ambaye amependekeza kupigwa marufuku kwa raia wa kigeni waislamu kuingia Marekani na baadhi ya viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya, Guteress amesema kwa kuwakataa wakimbizi hasa iwapo ni waislamu ni kudhihirisha wazi kuwa ni washirika wakubwa wa propaganda za wanamgambo wa IS na makundi mengine ya wanamgambo wenye itikadi kali.

Trump amulikwa

Mgombea Urais wa chama cha Democrats nchini Marekani Hillary Clinton siku ya Jumamosi alisema IS inatumia matamshi ya chuki yanayotolewa na Trump dhidi ya wahamiaji na waislamu kuwasaida wanamgambo hao kuwasajili wapiganaji wapya. Trump amekanusha madai hayo na kumuita Clinton muongo.

Mgombea Urais Marekani Donald Trump
Mgombea Urais Marekani Donald TrumpPicha: picture-alliance/dpa

IS ilifanya mashambulizi ya kigaidi mjini Paris mwezi Novemba na mtu na mkewe waliodai kuwa wafuasi wa IS katika jimbo la California nchini Marekani walifanya shambulizi katika kituo kimoja kilichoko San Bernadino tarehe mbili mwezi huu.

Mashambulizi hayo yalichochea onyo kutoka kwa baadhi ya wanasiasa barani Ulaya na Marekani kuwa huenda nchi zao zikakabiliwa na kitisho cha ugaidi kwa kuwapokea maelfu ya wahamiaji kutoka nchi zenye mizozo.

Majimbo kadhaa ya Marekani yalisema yatawafungia milango wakimbizi huku Trump akitaka waislamu kutoka nchi za kigeni kupigwa marufuku kuingia Marekani.

Mkuu huyo wa UNHCR amesema ulimwengu haupaswi kusahau kuwa wakimbizi ndiyo waathiriwa wa kwanza wa ugaidi na sio chanzo cha ugaidi na kuongeza kinachohitajik ni kuongezwa kwa kasi ya juhudi za kidiplomasia kuhakikisha kuna amani duniani.

Wakati huo huo, UNHCR na mashirika ya kutetea haki za binadamu yameihimiza Hungary kukomesha sera ambazo zinakuza kutovumiliana na chuki dhidi ya wahamiaji.

Wameishutumu kampeini iliyoanzishwa mwezi huu na serikali ya Hungary inayosema wakimbizi wengi wao kutoka Syria ni wahalifu na magaidi kutokana na imani zao za kidini na wanakotokea.

Hungary yaonywa kwa kuendeleza chuki

Hungary imechukua hatua kali dhidi ya wahamiaji ikiwemo kuweka ua katika mipaka yake kuwazuia wakimbizi kuingia nchini mwao. Waziri wa mambo ya nje wa Hungary Peter Szijjarto amekanusha madai hayo kuwa nchi yake inaendeleza chuki dhidi ya wahamiaji.

Wakimbizi wakiingia mjini Dobova, nchini Slovania
Wakimbizi wakiingia mjini Dobova, nchini SlovaniaPicha: Reuters/S. Zivulovic

Huku hayo yakijiri, Shirika la reli nchini Sweden limetangaza litasitisha baadhi ya huduma zake kuelekea na kutoka Denmark kama sehemu ya hatua ya kukabiliana na mzozo wa wakimbizi. Kuanzia mwezi ujao, kampuni za uchukuzi nchini humo zitatozwa faini iwapo zitawabeba abiria wasiokuwa na vitambulisho.

Serikali ya Sweden imeiuomba Umoja wa Ulaya kuiondoa kwa muda kutoka makubaliano ya nchi wanachama wa Umoja huo ya kusafiri kwa uhuru bila ya visa ujulikanao Schengen ili kuweza kukabiliana na ongezeko la wahamiaji wanaoingia nchini humo.

Takriban wahamiaji milioni moja wameingia Ulaya mwaka huu, wengi wao kutoka nchi zenye mizozo kama Syria, Iraq na Afghanistan.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri:Iddi Ssessanga