1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yasikitishwa na mashambulizi yanayoendelea Myanmar

19 Machi 2024

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaja kusikitishwa na taarifa za mashambulizi ya anga yanayoendelea katika vijiji vya jimbo la Rakhine nchini Myanmar.

https://p.dw.com/p/4dt3b
Myanmar | Maandamano
Wanajeshi wa Myanmar wakijiweka tayari kukabiliana na waandamanaji 2021Picha: AP/picture-alliance

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaja kusikitishwa na taarifa za mashambulizi ya anga yanayoendelea katika vijiji vya jimbo la Rakhine nchini Myanmar, ambapo wenyeji wameliambia shirika la habari la AFP kuwa zaidi ya watu 20 wameuawa hapo jana.

Mapigano yamelitikisa jimbo hilo la magharibi mwa Myanmar tangu Jeshi la Arakan (AA) liliposhambulia vikosi vya usalama mwezi Novemba mwaka jana, na hivyo kuvunja makubaliano ya usitishaji wa mapigano ambayo yaliheshimiwa kwa kiasi kikubwa tangu mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2021.

Mzozo wa hivi majuzi umesababisha maelfu ya watu kuyahama makazi yao huko Rakhine, ambako ukandamizaji wa kijeshi wa mwaka 2017 ulipelekea mamia ya maelfu ya Warohingya kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh.