UN yaiwekea vikwazo Eritrea | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 24.12.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

UN yaiwekea vikwazo Eritrea

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa laiwekea vikwazo Eritrea kutokana na tuhuma za kuwasaidia waasi wa Somalia.

Rais wa Eritrea, Isaias Afewerki.

Rais wa Eritrea, Isaias Afewerki.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limepitisha azimio la kuiwekea Eritrea vikwazo kwa sababu ya msaada ambao wajumbe wa baraza hilo wanasema nchi hiyo imekuwa ikiwapatia wanamgambo wa Kiislamu nchini Somalia na kukataa kuwaondoa wanajeshi wake katika mpaka wa nchi hiyo na Djibouti, ambao una mgogoro.

Azimio hilo lililopitishwa na wanachama 13 kati ya 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaiwekea moja kwa moja Eritrea vikwazo vya silaha, pamoja na kuzuia fedha na mali za viongozi wa kisiasa na kijeshi wanaodaiwa kuwasaidia waasi hao. Marekani na mataifa mengine yanaituhumu Eritrea kwa kuwapatia msaada wa fedha na silaha kundi la waasi la al-Shabaab, linalopigana kuiondoa madarakani serikali ya mpito ya Somalia inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, tuhuma ambazo Eritrea imerudia kukanusha.

Nchi 2 ambazo hazikuunga mkono azimio hilo

Libya ambayo haina kura ya turufu katika baraza hilo, ilipiga kura kulipinga azimio hilo, huku China ambayo ina kura ya turufu haikupiga kura. Katika mjadala wa baraza hilo, mjumbe wa Libya, Ibrahim Dabbashi, alisema azimio hilo limeidhinishwa haraka sana na anaamini kwamba suala hilo lingehairishwa hadi baada ya mkutano wa Umoja wa Afrika mwezi ujao. Naye Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Susan Rice amesema vikwazo hivyo siyo kwamba mlango umefungwa kwa Eritrea, lakini ni nafasi nyingine kwa nchi hiyo kuwajibika zaidi kusaidia kulijenga upya eneo la Pembe ya Afrika.

Azimio hilo linaitaka Eritrea kuacha kutoa mafunzo ya kijeshi na kuyapatia silaha makundi ya wapiganaji na wafuasi wao likiwemo kundi la al-Shabaab, kwa lengo la kuvuruga amani katika eneo hilo na pia linaitaka nchi hiyo iliyopo katika Pembe ya Afrika kutatua mzozo wa eneo lililopo kwenye mpaka wa nchi hiyo na ile jirani ya Djibouti. Azimio hilo linasema kuwa vitendo vya Eritrea vinakwamisha amani na mapatano nchini Somalia pamoja na mzozo uliopo baina ya Djibouti na Eritrea unaotishia amani na usalama wa kimataifa. Hii ni mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kuiwekea Eritrea vikwazo, taifa ambalo lilipata uhuru wake kutoka kwa Ethiopia mwaka 1993.

Uganda ndio iliwasilisha azimio hilo

Wanadiplomasia wanasema Uganda ambayo ina wanajeshi wa kulinda amani Somalia yanayowalenga al-Shabaab, iliwasilisha muswada wa azimio hilo baada ya Umoja wa Afrika kulitaka baraza hilo la usalama la Umoja wa Mataifa kuiadhibu Eritrea kwa tuhuma hizo za kuwaunga mkono wanamgambo wa Somalia. Balozi wa Eritrea kwenye Umoja wa Mataifa, Araya Desta amelielezea azimio hilo kuwa la aibu na kwamba linaegemea uongo uliotungwa na Ethiopia pamoja na Marekani.

Desta amesema nchi yake haijawahi kuwaunga mkono wapiganaji wowote au kundi lolote la upinzani nchini Somalia kwa sababu Wasomali ni ndugu zao. Ethiopia ambayo ni mpinzani wa Eritrea, iliivamia Somalia mwaka 2006 ikiungwa mkono kimya kimya na Marekani kwa ajili kuwaondoa wapiganaji wa muungano wa mahakama za Kiislamu waliokuwa wakiudhibiti mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, ingawa iliwaondoa wanajeshi wake mwanzoni mwa mwaka huu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE)

Mhariri: Othman Miraji

 • Tarehe 24.12.2009
 • Mwandishi Kabogo, Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LCn9
 • Tarehe 24.12.2009
 • Mwandishi Kabogo, Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LCn9
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com