1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Vifo vya watoto vimepungua, athari bado ipo

13 Machi 2024

Umoja wa mataifa umeripoti kwamba idadi ya watoto walioaga dunia kabla ya umri wa miaka mitano ilipungua na kufikia kiwango cha chini kabisa katika mwaka 2022.

https://p.dw.com/p/4dSej
Shirika la UNICEF| Huduma kwa watoto Sudan
Wanawake na watoto wao waliokimbia vita katika eneo la Tigray nchini Ethiopia wakipata huduma ndani ya hema la UNICEF.Picha: Nariman El-Mofty/AP Photo/picture alliance

Hiyo ni mara ya kwanza ambapo idadi ya vifo vya watoto ilikuwa chini ya milioni tano.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto, UNICEF kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Benki ya Dunia, inakadiria kuwa takriban watoto milioni 4.9 walikufa kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano katika mwaka 2022 ikiwa ni kiwango cha kihistoria cha vifo vya watoto kuwa chini ya milioni tano kwa mara ya kwanza.

Soma pia: Watoto 68,000 Nepal wahitaji msaada

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesema kwamba idadi hii imefanikiwa kutokana na juhudi za pamoja kati ya wakunga na wahudumu wa afya kuwasaidia kina mama kujifungua salama, kuwachanja watoto dhidi ya magonjwa hatari na kuzisadia familia.

Maendeleo yameonekana hasa katika nchi zinazoendelea kama Malawi, Rwanda na Mongolia, ambako vifo vya watoto wachanga vimepungua kwa zaidi ya asilimia 75 tangu mwaka 2000.

Akizungumza na shirika la habari la AFP, Mkurugenzi wa Afya wa UNICEF Helga Fogstad, amesema ni habari njema na kubwa kwamba tumefikia kiwango cha kihistoria cha vifo vya watoto chini ya miaka mitano, chini ya milioni 5 kwa mara ya kwanza.

"Kuna hatari ya suala la kukosekana kwa usawa. Na ni suala linalohusu uchumi na linahusu hali mbaya ya migogoro na mazingira tete ya kibinadamu.

Fogstad hata hivyo ameonya kuwa maendeleo hayo "yako katika hali tete" na hayana usawa kwa maana kuwa yanaweza kurudishwa nyuma wakati wowote.

"Lakini nina imani sana kwamba ikiwa tutapata uangalizi wa kutosha juu ya suala hili muhimu, itawezekana kuharakisha juhudi za kufikia lengo mnamo 2030. Na hiyo itahitaji msaada na usaidizi wa ziada kutoka kwa washirika mbalimbali." Aliongeza Fogstad.

Ukosefu wa usawa

Hema la Shirika la UNICEF
Mkimbizi kutoka Tigray Rega Tsfay mwenye umri wa miaka 38, akiwa na mwanawe mwenye umri wa miezi 3, mwenye utapiamlo wakipumzika ndani ya hema linalosimamiwa na UNICEF.Picha: Nariman El-Mofty/AP Photo/picture alliance

Idadi hizo zinaonyesha kukosekana kwa usawa duniani kote, kwani eneo la Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara lilichangia nusu ya vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kwa mwaka 2022.

Soma pia: UNICEF yaomba dola bilioni 9.3 za kusaidia watoto 2024

Imetajwa kwamba mtoto anayezaliwa katika nchi zilizo na vifo vingi vya watoto, kama vile Chad, Nigeria au Somalia, ana uwezekano mara 80 zaidi wa kufa kabla ya kufikisha miaka mitano kuliko aliyezaliwa katika nchi zilizo na viwango vya chini vya vifo vya watoto, kama vile Finland, Japan na Singapore.

Ripoti hiyo imebainisha kwamba watoto walio kati ya umri wa mwezi mmoja na miaka mitano, wanapoteza maisha kutokana na magonjwa ya kupumua, malaria na kuharisha licha ya kwamba maradhi hayo yanaweza kuepukika.

Ili kufikia lengo la Umoja wa Mataifa la kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano hadi 25 kwa kila watoto 1,000 wanaozaliwa ifikapo mwaka 2030, nchi 59 zitahitaji uwekezaji wa haraka katika afya ya watoto.