1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine na pengo la mshikamano katika jamii magazetini

13 Mei 2014

Hali Ukraine,wimbi la wakimbizi na mshikamano miongoni mwa jamii ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo

https://p.dw.com/p/1Bymn
Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ziarani mjini Kiev , katika juhudi za kuzileta katika meza ya majadiliano pande zinazohasimiana.Anaamkiana na waziri mkuu wa Ukraine YazenjukPicha: Reuters

Tuanzie Ukraine ambako mbali na walimwengu kukosoa kile kinachoitwa kura ya maoni,juhudi za kuyaleta pamoja makundi yanayohasimiana pia zinaendelezwa.Gazeti la "Mittelbayerische Zeitung" la mjini Regensburg linaandika"Tunaweza kusema hii ni faraja kwamba Uswisi ndiyo mwenyekiti wa sasa wa jumuia ya Usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE.Hakuna nchi yoyote nyengine ya Ulaya yenye maarifa makubwa zaidi ya mfumo wa shirikisho.Na hapo Ukraine inaweza kufaidika.Kwasababu nchi hiyo,na ikiwa itataka kuendeleza umoja wake,basi haitakuwa na budi isipokuwa kuachana na mfumo wa sasa ambao madaraka yanatuwama mahala pamoja.Pekee katika mfumo wa shirikisho ambapo kila jimbo litakuwa na uwezo mkubwa wa kujiamulia mambo yake ndipo Ukraine inayolega lega, itakapoweza kunusurika.Lakini ili ufumbuzi kama huo upatikane,panahitajika kwanza mdahalo wa taifa.Bado si dhahir kama uongozi wa mjini Kiev na waasi wanaoelemea upande wa Urusi watakubali kukewti katika meza moja ya mazungumzo.

Pengo katika mshikamano miongoni mwa jamii linazidi kupanuka

Uchunguzi uliofanywa na wakfu wa Bertelsmann kuhusu mshikamano katika jamii umebainisha hali hiyo inapewa umuhimu mkubwa zaidi katika sehemu ya iliyokuwa Ujerumani magharibi ya zamani,ikilinganishwa na sehemu ya mashariki.Gazeti la "Badische Neuste Nachrichten" linajaribu kuitathmini hali hiyo na kuandika:"Kwamba mshikamano katika majimbo mepya ya Ujerumani, si mkubwa hivyo miaka 25 baada ya kuporomoka ukuta,si suala la vivi hivi tu.Kule ambako idadi ya wasiokuwa na kazi,bado inagonga na baadhi ya wakati kupindukia asili mia 10,watu wanakuwa na mambo mengine yanayowashughulisha zaidi .Wanahisi kana kwamba muungano umewaondoa patupu na kwa namna hiyo wanaitwika nchi nzima jukumu la hali yao na kutoa joto la moyo wao kama uchunguzi wa wakfu wa Bertelsmann ulivyobainisha.Picha iliyobainishwa na wakfu wa Bertelsmann iko mbali na ukweli halisi wa hali ya mambo-kwasababu mwanya kati ya mashariki na magharibi unazidi kupanuka badala ya kupungua.

Wakimbizi wa kiuchumi

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu wimbi la wahamiaji kutoka nchi za mashariki na kusini mwa ulaya wanaoingia katika nchi za Umoja wa ulaya kutafuta hali bora ya maisha.Gazeti la "Bild" linajaribu kuangalia sababu zinazowafanya wakimbizi hao kupendelea zaidi kujua nchini Ujerumani.Gazeti linaendelea kuandika:"Huduma za jamii wanazopatiwa wahamiaji kutoka sehemu za mashariki na kusini mwa ulaya nchini Ujerumani wanahisi ni kubwa ajabu.Nchi ambayo wakaazi wake wasiojimudu wanapatiwa hadi Euro 215 kama fedha za kuwatunza watoto na wazee ,mahala wanakopatiwa huduma za afya bila ya kulipia chochote pamoja na kulipwa Euro 391 kwaajili ya mahitaji yao ya mwezi mmoja pamoja pia na mahala bure pa kuishi.Kwao wao wanahisi hii ni pepo ya duniani.Kwa hivyo si ajabu wanapoongozana kwa wingi na kuingia Ujerumani.Hebu tujiulize sisi tungefanya nini tungejikuta katika hali kama yao,bila ya kazi wala matumaini ya maisha bora?Tatizo lakini ni kwamba nchi yetu imezidiwa na hasa inapotaka kujigeuza kituo cha huduma za jamii cha Umoja wa Ulaya.Na hilo wanasiasa wa mjini Brussels sawa na wanasheria wa Ulaya wanabidi hatimae walitambue .

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri . Mohammed Abdul-Rahman