1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaendeleza mashambulizi Gaza

28 Machi 2024

Israel imefanya mashambulizi ya anga na kushambulia takriban nyumba nne huko Rafah, ambapo watu 11 wa familia moja waliuawa, na hivyo kuibua hofu miongoni mwa Wapalestina zaidi ya milioni 1.2 waliokimbilia eneo hilo.

https://p.dw.com/p/4eChQ
Gaza- Mashambulizi ya Israel
Mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa GazaPicha: Ismael Mohamad/UPI Photo/IMAGO

Shambulio jingine huko Rafah limesababisha vifo vya mwanamke mmoja na mtoto. Eneo la Magharibi mwa Ukanda wa Gaza, watu wengine saba wameuawa. Jeshi la Israel linadai kuwalenga wanamgambo wa Hamas ambao imesema wanatumia majengo ya raia na hospitali.

Taarifa inayokanushwa na kundi la Hamas ambalo linazingatiwa na Umoja wa Ulaya, Ujerumani na mataifa mengine ya Magharibi kuwa kundi la kigaidi.

Soraya Ali ni mkuu wa masuala ya habari katika shirika la kimataifa la kuwalinda watoto la Save the Children, kwa sasa yuko Rafah na ameiambia DW kwamba  hali ya kibinadamu kusini mwa Gaza ni ya kutisha . Amesema jumla ya watoto 13,700 wameuawa, wengine wanaishi katika mazingira magumu mitaani huku wakikabiliwa na magonjwa na utapiamlo.

 Bi Ali amesema mashambulizi ya Israel huko Rafah ni sawa na jinamizi kwa kuwa watu hawana mahali popote pa kwenda.

Gaza I Mtoto akipokea msaada wa kiutu Rafah
Mtoto wa Kipalestina akiondoka na msaada wa chakula huko RafahPicha: Abed Rahim Khatib/dpa/picture alliance

Vurugu zimeongezeka pia katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel, ambapo Wapalestina watatu wameuawa na wengine wanne wamejeruhiwa kufuatia mashambulizi ya Israel huko Jenin. Hayo ikiwa ni kulingana na wizara ya Afya ya Palestina.

Soma pia: Mashambulizi makali ya Israel yapiga kusini mwa Gaza, katikati ya ongezeo la kitisho cha njaa

Wizara hiyo inayodhibitiwa na Hamas imesema takriban Wapalestina 32,000 wameuawa huko Gaza tangu kuanza kwa mzozo huu Oktoba 7 mwaka jana, huku maelfu ya wengine wakiaminika kuwa wamefukiwa chini ya vifusi. Zaidi ya asilimia 80 Wapalestina wapatao milioni 2.3 wameyakimbia makazi yao, huku wengi wao wakiwa katika hatari ya kukabiliwa na njaa.

Mashirika ya misaada yamekuwa yakitoa miito ya kuongeza kasi ya uwasilishaji wa misaada huko Gaza . Kwa sasa misaada huwasilishwa Gaza kupitia angani, ardhini na majini.

Ikulu ya White House imetoa salamu za rambirambi jana usiku kufuatia tukio la watu 12 waliopoteza maisha huko Gaza wakijaribu kuufikia msaada uliodondoshwa na ndege kwenye maji .

Israel yakabiliana na Hezbollah katika mpaka wake na Lebanon

Lebanon- Mashambulizi ya Israel huko Lebanon
Watu wa Lebanon wakielekea kwenye mazishi ya watu waliouawa kufutia mashambulizi ya Israel katika kijiji cha Hebbariye: 27.03.2024Picha: Mohammed Zaatari/AP/picture alliance

Kundi la Hezbollah la nchini Lebanon linalofadhiliwa na Iran, limefyetua makombora kuelekea kaskazini mwa Israel katika mji wa Kiryat Shmona na kuua raia mmoja. Israel ilifanya pia mashambulizi ya kulipiza kisasi katikaa eneo la mpakani na Lebanon na kusababisha vifo vya watu 9.

Vyombo vya habari vya Lebanon vimeripoti kwamba mashambulizi hayo ya usiku wa kuamkia leo yalikilenga kituo cha matibabu cha kundi la wapiganaji wa Kisunni cha al-Jamaa al-Islamiya. Jeshi la Israel limedai kukilenga kituo cha kijeshi na kwamba waliwaua wanamgambo pekee.

Taarifa zinabaini kuwa mapigano makali kati ya jeshi la Israel na  wanamgambo wa Hezbollah wa Lebanon  tayari yamesababisha vifo vya watu 16. Waangalizi wanahofia kutanuka kwa mzozo huu.

(Vyanzo: Mashirika)