1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yaitaka Iran kuiachia meli yake ya mafuta

Sekione Kitojo
22 Julai 2019

Uingereza imerudia madai yake kwa Iran kuiachia meli ya mafuta inayopeperusha bendera ya Uingereza iliyoikamata katika eneo la  Ghuba, wakati serikali ya waziri mkuu May ikifanya kikao juu ya kujibu hatua hiyo ya Iran.

https://p.dw.com/p/3MYU0
Britischer Tanker Stena Impero
Picha: picture-alliance/AP Photo/Stena Bulk

Waziri  wa  mambo  ya  kigeni  Jeremy Hunt  anapanga kulifahamisha  bunge  siku  ya  Ijumaa  kukamatwa kwa  meli  ya mafuta  ya  Stena Impero pamoja  na  wafanyakzi  wake 23, ambao hivi  sasa  wako  katika  bandari  ya  Iran  yenye   ulinzi  mkali.

Pia  leo Jumatatu, Iran ilitoa  vidio  mpya  inayoonesha  wafanyakazi wa  meli  hiyo  kwa  mara  ya  kwanza, ikiwa  ni  jaribio  la  kuonesha kwamba  hawajadhurika.

Öltanker Stena Impero
Meli ya kubebea mafuta ya Uingereza Stena Impero katika eneo ambalo halikutajwaPicha: picture-alliance/AP Photo/B. M. Karatzas

Hakuna hata  raia mmoja  wa  Uingereza, lakini  wengi  wao  ni kutoka India   na  pia  Ufilipino, Urusi na  raia  wa  Latvia.

Msemaji  rasmi  wa May , James Slack , amesema  Iran imeikamata meli  hiyo kwa  kutumia visingizio vya  uongo na  ni kinyume  na sheria na  inahitaji kuiachia pamoja  na  wafanyakazi wake mara moja.

Amesema  hakuna  mpango  wa  kuzipatia meli  zote  zinazotembea zikipeperusha  bendera  ya  Uingereza msaada  wa  kuzisindikiza, kwasababu  ya wingi  wa  meli  hizo. Lakini  amekana  kuwa kubana matumizi  kumesababisha  jeshi  la  majini  kuwa  dogo mno.

Uingereza inatafakari  njia  mbali  mbali  za  kuongeza mbinyo  wa kidiplomasia  na  kiuchumi kwa  Iran, lakini  maafisa  wanasema operesheni  za  kijeshi halifikiriwi  kwa  wakati  huu. Uingereza  pia inatafuta  kuungwa  mkono  kutoka  kwa  washirika  muhimu  wa Ulaya  katika  juhudi  za  kuliweka  eneo  la  mlango  bahari  wa Hozmuz wazi  kwa  ajili  ya  meli.

Donald Trump bei Theresa May
Theresa May waziri mkuu wa Uingereza (kushoto) akiwa na rais wa marekani Donald Trump (kulia)Picha: Reuters/P. Nicholls

Uchochezi wa mzozo

Waziri  wa  mambo  ya  kigeni  wa  Ujerumani Heiko Maas  amesema ana  wasiliana  kwa  karibu  na  mataifa  ya Umoja  wa  Ulaya  kama Ufaransa  na  Uingereza  katika  mzozo  na  Iran. Amesema  mataifa ya  magharibi  hayapaswi  kuuchochea  zaidi mzozo  huu.

"Kwetu sisi  ni  muhimu kwamba, pamoja  na  hatua  za  kuzuwia hatari  katika mlango bahari wa  Hormuz, kadi ya  kidiplomasia ni lazima iendelee  kutumika. hususan, naamini  kwamba  ni  muhimu kuzileta  nchi  za  ghuba katika  meza moja katika wakati  fulani kujadili masuala  ya  usalama baharini. Kila  kitu ni  lazima kiwekwe akilini  na  tusichukua  hatua  ambazo zitachangia  katika kuuchochea  mzozo huu. Kile  tunachohitaji ni kutouchochea mzozo. Na hili  pia ni wazo  la  wenzetu wa Uingereza  na  Ufaransa."

Außenminister Deutschland Afghanistan Heiko Maas Salahuddin Rabbani
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko MaasPicha: picture-alliance/AA/C. Karadag

Wakati  huo  huo mwanadiplomasia  wa  ngazi  ya  juu  wa  Oman atakwenda  Iran mwishoni  mwa  juma  hili, mnamo  wakati ambapo Oman imekuwa na uhusiano  mzuri  na  Iran katika  wakati wote  wa mizozo  mbali  mbali  ya  kikanda, na kuruhusu wakati  fulani  kuwa mpatanishi, ikiwa  ni  pamoja  na hata  katika  mizozo  inayoihusu Marekani  na  mataifa ya ghuba.

Rais wa Marekani  nae  amekana  madai ya Iran kuwa  imevunja genge  ya  makachero wa  CIA  na  kuwakamata  watuhumiwa 17 waliodaiwa  kuwa  wana  mahusiano  na  shirika  la  ujasusi  la Marekani CIA.