Uingereza yaionya Libya kutosherehekea mwaka mmoja tokea kuachiwa Megrahi | Habari za Ulimwengu | DW | 20.08.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Habari za Ulimwengu

Uingereza yaionya Libya kutosherehekea mwaka mmoja tokea kuachiwa Megrahi

Leo ni mwaka mmojka tokea kuachiwa huru kwa mhusika wa shambulio la bomu dhidi ya ndege ya abiria ya Marekani katika anga la Lockerbie, Abdelbaset Ali Mohammed al-Megrahi ,

Abdel Baset al-Megrahi, mwenye suti nyeusi aliporeja Libya mwaka jana akiwa na kiongozi wa Libya Seif al-Islam Gadhafi kulia

Abdel Baset al-Megrahi, mwenye suti nyeusi aliporeja Libya mwaka jana akiwa na kiongozi wa Libya Seif al-Islam Gadhafi kulia

Uingereza imeionya Libya kuwa sherehe zozote za kuadhimisha siku hiyo, zitakuwa , ni kinyaa , zinazoonyesha dharau na kutokuwa na hisia.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Uingereza imetoa wito wa kujizuwia huku kukiwa na hofu kuwa inawezekana kutokea hali kama iliyotokea mwaka jana wakati Abdelbaset Ali Mohammed al-Megrahi aliporejea nyumbani na kupokewa kama shujaa nchini Libya baada ya kuachwa huru.

Serikali ya Scotland , ambayo ndiyo iliyochukua uamuzi wa kumuachia huru mshambuliaji huyo kutoka Libya , pia inaripotiwa kuitaka Libya kujiepusha kufanya sherehe mwaka huu, ikisema kuwa matukio yoyote ya hadhara yatakayofanyika kwa heshima ya Megrahi yatalaaniwa.

Serikali ya Scotland iliyokabidhiwa mfungwa huyo ilimwachia huru kwa misingi ya kumuonea huruma hapo August 20 mwaka jana, ikisema kuwa ni mgonjwa sana akiwa na saratani ya tezi za kibofu na huenda ana weza kuishi kwa muda wa miezi mitatu tu.

Lakini Megrahi bado yu hai hadi leo nchini mwake, na kuzusha hasira miongoni mwa ndugu wengi wa watu 270 ambao wameuwawa wakati ndege ya shirika la ndege la Marekani, Pan Am ilipolipuka katika anga ya Lockerbie nchini Scotland Desemba mwaka 1988.

Wakala huyo wa zamani wa ujasusi , mwenye umri wa miaka 58, alikuwa mtu pekee aliyehukumiwa kuhusiana na uovu huo , na aliachiliwa baada ya kutumikia kifungo cha miaka minane kati ya miaka 20 aliyohukumiwa.

Kuachiwa kwake kumeleta mtikisiko katika uhusiano baina ya Marekani Uingereza na hata baina ya serikali za Scotland na Uingereza. Scotland imekuwa ikitetea uamuzi huo, wakati Uingereza ikisisitiza kuwa inaamini uamuzi huo ulikuwa ni makosa.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni mjini London jioni ya Alhamis ameitaka Libya kutofanya sherehe kwa heshima ya mtu , aliyehukumiwa kwa kufanya tukio baya la kigaidi katika historia ya Uingereza.

Hususan katika siku ya leo ya maadhimisho tunatambua maumivu makali yanayoendelea ambayo yamesababishwa kwa wahanga, kutokana na kuachiliwa huru kwa Megrahi, nchini Uingereza na Marekani , msemaji huyo amesema.

Sherehe zozote za kuachiwa kwa Megrahi zitakuwa ni kinyaa, zinazoonesha dharau na zinazoonesha kutokuwa na hisia kwa familia za wahanga.

Ameongeza kuwa tumeweka wazi wasi wasi wetu kwa serikali ya Libya. Balozi wa Uingereza nchini Libya, Richard Northern, ameweka wazi kwa maafisa waandamizi wa serikali ya Libya kuwa tukio lolote la hadhara kwa heshima ya Megrahi linaweza kuharibu uhusiano baina ya nchi hizo mbili, limeripoti gazeti la Guardian nchini Uingereza.

Waziri wa sheria wa Scotland Kenny MacAskill, ambaye alichukua uamuzi huo kumuachia huru al-Megrahi, ametetea hatua hiyo jana , akisema , ulikuwa ni uamuzi ambao alipaswa kuuchukua.

Mwandishi : Sekione Kitojo /AFPE

Mhariri: Aboubakary Liongo

 • Tarehe 20.08.2010
 • Mwandishi Aboubakary Jumaa Liongo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OsSX
 • Tarehe 20.08.2010
 • Mwandishi Aboubakary Jumaa Liongo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OsSX
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com