1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza kulegeza sheria kuhusu corona

Tatu Karema
5 Julai 2021

Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson anatarajiwa kutangaza mipango ya kuondoa sheria inayowalazimu watu kuvaa barakoa na hatua ya kuweka umbali wa mtu mmoja hadi mwingine.

https://p.dw.com/p/3w3tS
Großbritannien Premierminister Boris Johnson
Picha: House of Commons/PA/picture alliance

Johnson amesema ataelezea jinsi nchi hiyo itakavyojifunza kuishi na virusi hivyo haya yakiwa mabadiliko makubwa kutoka kwa kiongozi ambaye awali aliutaja ugonjwa wa COVID-19 kama adui anayepaswa kuangamizwa. Kabla ya mkutano na waandishi wa habari utakaopeperushwa kwa njia ya televisheni siku ya Jumatatu, Johnson aliashiria kuwa sheria za lazima zitabadilishwa baada ya Julai 19 siku inayotajwa na vyombo vya habari vinavyoegemea mrengo mkali wa kulia kuwa ni siku ya ''Uhuru''.

Johnson ameongeza kuwa, wanapoanza kujifunza kuishi na virusi vya corona, lazima wote waendelee kuwa waangalifu dhidi ya athari za ugonjwa wa COVID-19 na kufanya maamuzi bora wanapondelea na maisha yao ya kawaida. Ujumbe wa Johnson  utapongezwa na wabunge katika chama tawala cha kihafidhina kinachoongoza nchini humo wasiopendelea kufungwa kwa nchi hiyo kwa sheria za kudhibiti kuenea kwa maambukizo ya virusi hivyo wanaosema kuwa hasara ya kiuchumi na kijamii zinazidi manufaa ya afya ya umma.

Wito wa tahadhari watolewa

 Lakini maafisa wa afya ya umma na wanasayansi wamehimiza kuweko kwa tahadhari na kusema kuondoa sheria ya kuvaa barakoa na kuweka umbali wa mtu mmoja hadi mwingine  huenda kukasababisha hatari. Mwanasaikolojia Stephen Reicher, ambaye ni mwanachama wa kamati ya serikali ya ushauri wa kisayansi, amesema kuwa mikakati ya uthibiti dhidi ya virusi hivyo inapaswa kudumishwa.

Brüssel EU Gipfel | Xavier Bettel
Xavier Bettel- waziri mkuu wa LuxembourgPicha: Dursun Aydemir/AA/picture alliance

Wakati huo huo, waziri mkuu wa Luxembourg Xavier Bettel amelazwa hospitalini kwa uchunguzi wa kimatibabu kama hatua ya kinga baada ya kuthibitishwa kupata maambukizo ya virusi hivyo.

Afisa mmoja wa serikali ya Luxembourg ambaye hakutaka kutambulishwa, amesema hakujakuwa na habari mpya baada ya Bettel kulazwa hospitalini kwa masaa 24 ya uchunguzi wa kimatibabu hapo jana Jumapili. Bettle alitangaza kupata maambukizo ya virusi vya corona baada ya kuhudhuria mkutano wa siku mbili wa Umoja wa Ulaya pamoja na viongozi wengine 26 wa Umoja huo. Waandaji wa mkutano huo wamesema wanaamini kwamba mikakati yote ya kudhibiti maambukizo ilikuwa imezingatiwa wakati wa mkutano huo. Kufikia sasa hakuna kiongozi mwengine aliyethibitishwa kupata maambukizo.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wamekuwa wakikabiliwa na hatari ya kusambaza virusi vya corona katika moja ya mikutano yake mingi kwa muda wa mwaka mmoja sasa. Mikutano yao mingi huandaliwa kwa njia ya video na viongozi hao hulazimika kukusanyika katika makao yao makuu nchini Ubelgiji wanapohitaji kuzungumzia masuala muhimu yanayohitaji mazungumzo ya muda mrefu ya ana kwa ana.