1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhamiaji wachafua tena hali ya utulivu wa kisiasa Ujerumani

Caro Robi
6 Septemba 2018

Hali ya utulivu katika kambi ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel inaonekana kuchafuka tena baada ya waziri wa mambo ya ndani mwenye misimamo mikali kuhusu uhamiaji Horst Seehofer kuyatetea maandamano ya vurugu.

https://p.dw.com/p/34RL7
Deutschland, Berlin: Bundeskanzlerin Angela Merkel (CDU) und Horst Seehofer (CSU), Bundesminister des Innern, für Bau und Heimat, nehmen an der Plenarsitzung im Deutschen Bundestag
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Seehofer amelitaja suala la uhamiaji chanzo cha matatizo yote ya kisiasa. Hayo yanakuja miezi miwili tu tangu kushuhudiwa msukosuko mwingine katika serikali ya mseto ya Ujerumani uliosababishwa na waziri huyo wa mambo ya ndani wa Ujerumani aliyetishia kuisambaratisha serikali kutokana na suala tete la uhamiaji.

Baada ya miezi kadhaa ya malumbano, muafaka ulifikiwa kati ya Kansela Merkel na Seehofer na hivyo kupelekea suala hilo la uhamiaji kutulia kwa kipindi cha karibu miezi miwili iliyopita.

Uhamiaji wasababisha mpasuko Ujerumani

Lakini kufuatia kisa cha kuuawa kwa kudungwa kisu kwa mjerumani mwenye umri wa miaka 35  na wanaume wawili kutoka Syria na Iraq mjini Chemnitz mwezi uliopita, suala hilo la uhamiaji limezuka tena.

Hannover - Demonstration "Wir sind mehr" #wirsindmehr
Maandamano ya umma mjini ChemnitzPicha: picture-alliance/dpa/J. Stratenschulte

Wafuasi wa makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia na raia wa mji huo wa Chemnitz ulioko mashariki mwa Ujerumani waliandamana kwa siku kadhaa baada ya mauaji hayo, huku kukiripotiwa visa vya kushambuliwa kwa watu waliodhaniwa kuwa raia wa kigeni.

Kama waziri wa mambo ya ndani, Seehofer amekuwa akitarajiwa kujitokeza na kulaani maandamano ya ghasia, mashambulizi ya raia kigeni na kuibuka kwa matukio ya kinazi lakini amenyamaza kimya hadi siku ya Alhamisi ambapo alivunja kimya chake kwa kusema anatamani angeweza kujiunga na maandamano hayo ya kuwapinga wahamiaji.

Akihojiwa na gazeti la Rheinische Post, kiongozi huyo wa jimbo la Bavaria, amesema kuana ghadhabu miongoni mwa umma kuhusiana na mauaji ya Chemnitz ambayo anaelewa, akiongeza kuwa kama hangekuwa waziri, pia naye angeandamana kama raia.

Seehofer amesisitza haendekezi kabisa watu wanaotumia fursa ya kuandamana kufanya ghasia au kushambulia watu wakiwemo polisi.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa sera ya Merkel ya kuwapokea wahamiaji na wakimbizi, amesema anaelewa hasira zilizochochea maandamano na kutilia mkazo hoja yake kuwa suala la uhamiaji ndiyo chanzo cha matatizo yote ya kisiasa yanayoikumba Ujerumani, jambo ambalo amekuwa akilisema kwa miaka mitatu iliyopita, tangu Merkel kufungua mipaka ya Ujerumani kuwaruhusu zaidi ya wahamiaji milioni moja kuingia nchini humo.

Merkel ailaumu AfD kwa kuchochea chuki

Matamshi hayo ya Seehofer yanafanana na ya mwenzake wa Italia Matteo Salvini ambaye wiki hii alisema Merkel hakuona uzito wa matatizo yajayo ya kuwaruhusu wahamiaji kuingia Ulaya. Chama cha Seehofer Christian Social Union CSU ambacho ni chama ndugu na cha Merkel Christian Democratic Union CDU kinakabiliwa na uchaguzi jimboni Bavaria mwezi ujao.

Berlin Bundeskanzlerin Angela Merkel Mimik
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/Hannibal

Kutokana na ushindani mkali kutoka kwa chama cha mrengo wa kulia kinachowapinga wageni Ujerumani cha Alternative Für Deutschland AfD, CSU kupitia Seehofer kimekuwa kikionekana kutumia suala la uhamiaji kama fimbo ya kutofautiana na Merkel na wakati huo huo, kuitumia kama chambo cha kuwavutia wapiga kura.

Kiongozi wa AfD Alexander Gauland amemtetea Seehofer akiliambia gazeti la Neue Osnabrücker kuwa, Seehofer yuko sahihi kuhusu tathmini yake juu ya sera za Merkel za uhamiaji.

Merkel amesema uhamiaji una changamoto ndiyo, lakini pia kuna mafanikio yatokanayo na uhamiaji, akiongeza kuwa ameona matukio ya Chemnitz ambayo bila shaka yamejaa chuki na kuteswa kwa watu wasio na hatia.

Merkel amekishutumu chama cha AfD kwa kutumia kisingizio cha maandamano ya vurugu kuchochea chuki za kibaguzi.

Uhamiaji umesababisha mpasuko mkubwa Ujeumani na kudhoofisha umaarufu wa Merkel ambaye ameiongoza Ujerumani kwa miaka 13. Wengi wa wachambuzi wanasema muhula huu wa nne ndiyo utakuwa wa mwisho kwa Kansela huyo wa Ujerumani.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman