1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhaba wa sukari Tanzania waleta hofu kwa wakaazi

19 Februari 2024

Kuendelea kukosekana kwa bidhaa muhimu nchini Tanzania kama vile sukari kumezuwa wasiwasi kwa wananchi wengi wanaohofia kuzidiwa na ukali wa maisha. Serikali ya taifa hilo la Afrika mashariki imesema linashughuli hilo.

https://p.dw.com/p/4cZFJ
Mkulima wa zao la mua
Mkulima wa zao la mua akivuna kwa ajili ya kupeleka kiwandani kwa ajili ya uchakataji zaidiPicha: Kent Gilbert/picture alliance

Mkuu wa mkoa wa jiji kuu la kiuchumi na kibiashara, Dar es Salaam, Albert Chalamila, anasema wakaazi wa mkoa wake wana hofu licha ya juhudi za serikali kukabiliana na hali hiyo. 

Ukiweka kando masuala kama mgao wa umeme unaoendelea kushuhudiwa sasa pamoja na kuadimika kwa dola ya Marekani katika mzunguko wa soko, suala la uhaba wa sukari ni jambo linalogonga vichwani mwa wengi  na ambalo pia linazidisha mtihani kwa wanasiasa.

Bidhaa hiyo imeadimika katika maeneo mengi ya nchi. Hata pale mahala inapopatikana, basi bei yake inawaumiza wananchi. Kwa kipindi kifupi, bidhaa hiyo muhimu imepanda kutoka bei shilingi 2,800 na 3,000 kwa kilo hadi kufikia shilingi 4,500 mpaka 5,000 kwa kilo moja.

Soma pia:Soko la sukari la Umoja wa Ulaya kurekebishwa

Kumekuwa na sababu mbalimbali zinazotajwa kutokana na hali hiyo, lakini baadhi ya wananchi wanainyooshea kidole cha lawama serikali wakisema "inaachia mchezo wa danadana" kuhusu jambo hilo

"Kama sukari ndani haipo kwanini watu wasiingize sukari nchini? Alisema mmoja wa wananchi alipozungumza na DW mjini Dar es salaam.

Mwananchi huyo aliongeza kuwa kwa sasa familia nyingi za Kitanzania suala la chai sasa limekuwa ni hadithi na wengi wanatumia chumvi kama mbadala.

Madai ya kuficha bidhaa ya sukari sokoni

Ripoti zinasema katika baadhi ya mikoa bidhaa hiyo inapatikana, lakini inafichwa na wajanja wachache wenye lengo na kujinufaisha kibiashara. Katika maeneo mengine, hali ni mbaya zaidi kutokana na kuendelea kuadimika kwake.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, hii leo amekiri mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisema wananchi wa mkoa wake wamekumbwa na hofu kutokana na kuendelea kuadimika kwa bidhaa hiyo.

Maandalizi ya ramadhani katika mfumuko wa bei ya vyakula

" Wananchi wetu bado wanalalamika lalamika huko pembeni. Jambo la kwanza ni kukosekana kwa sukari. Mkuu wa mkoa huyo alimwambia Waziri Mkuu Kaasim Majaliwa .

Katika hatua nyingine, Mamlaka ya Bei nchini imetoa amri ya bei elekezi ya sukari, ikitaja kuwa bei ya jumla ni shilingi 2,600 hadi  shilingi 2,900, huku bei ya rejareja kiwango cha chini kikianzia shilingi 2,700 hadi shilingi 3,200.

Kama sehemu ya utekelezaji wa hatua hiyo, afisa mwandamizi bodi hiyo, Fihili Omary Achi, ameendesha opresheni ya kukagua maduka kadhaa mkoani Kilimanjaro, kaskazini mwa nchi na kusema kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanapandisha bei kwa maslahi yao binafsi.

Soma pia:Sakata la sukari yenye zebaki Kenya

Mkanganyiko kuhusu bidhaa hiyo ya sukari umewasukuma pia wanasiasa wa upinzani kupeleka mashambulizi yao ya ukosoaji kwa serikali. (una sauti, au nukuu ya mwanasiasa yeyote wa upinzani? iweke)