Uganda yatakiwa kutoa kipaumbele kwa masuala ya Mazingira | Matukio ya Afrika | DW | 20.09.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Uganda yatakiwa kutoa kipaumbele kwa masuala ya Mazingira

Vijana wametoa rai kwa bunge la nchi hiyo kulipa kipaumbele suala la ulinzi wa mazingira, wakionya kuwa mabadiliko ya tabianchi yanatishia kusababisha majanga makubwa.

Hao ni wanafunzi wa shule za msingi na za sekondari katika mji wa Wakiso jirani na Kampala walioshiriki katika maandamano ya kutaka hatua zaidi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Maandamano hayo yaliyofanyika sehemu mbalimbali za nchi yanalenga kuzitaka mamlaka za kitaifa na kimataifa kutobaki tu katika gumzo la jinsi mabadiliko ya tabia nchi yanavyoathiri mazingira na maisha ya watu.

Vijana wamelezea kuwa japo kuna sheria nyingi za kulinda mazingira, kila kukicha sheria hizo hukiukwa na wawekezaji ambao wamevamia hata maeneo chepechepe.

Hiki ndicho chanzo cha majanga mbalimbali kama mafuriko, maporomoko ya ardhi na uhaba wa chakula unaowakumba watu sehemu mbalimbali za Uganda na kwingineko.

Nchini Uganda suala la kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki limegeuka kuwa la kisiasa. Mamlaka ya kitaifa ya Mazingira NEMA ilipojaribu kuchukua hatua hiyo, walikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa washiriki katika biashara hiyo.

Wanaharakati wataka sheria zibane shughuli zozote zinazosababisha ongezeko la joto

Kwa sasa ni Uganda tu ndiyo haijapiga marufuku ya moja kwa moja plastiki hizo hali ambayo inatatizo juhudi hizo katika mataifa jirani kwani wakati mwingine mifuko hiyo huvushwa mipaka kwa njia za panya.

Ni  kwa ajili hii ndipo wanaharakati ikiwemo vijana wanataka sheria zibane shughuli zozote ambazo zinasababisha ongezeko la joto, uchafuzi wa hewa, ukataji miti na kadhalika. Fred Onduli Machuru ni mratibu wa masuala ya kukabliana na tabianchi chini ya Umoja Mataifa.

Balozi wa shirika lijulikanalo kama Fridays for the Future Lillian Namugerwa amefafanua kuwa uhusika wa wanafunzi katika uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na tabia nchi una matokeo bora kwani watahamasisha jamii wanamoishi na pia kufahamu madhara ya siku zijazo. 

Vijana wa vyuo vikuu mjini Kampala wameandamana hadi bungeni ambako wamemkabidhi spika malalamiko yao kuhusu mabadiliko ya tabianchi

Maandamana hayo ya amani yamefanyika siku tatu kabla ya kongamano la Umoja Mataifa litakalofanyika New York Marekani.

Chanzo: DW Kampala