1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Uganda yasema imemkamata kamanda muunda mabomu wa ADF

19 Mei 2024

Jeshi la Uganda limesema leo Jumapili kwamba limemkamata kamanda wa kundi la waasi wa ADF inayeamini ni mtaalamu wa kuunda mabomu ambayo kundi hilo limekuwa likiyatumia kufanya hujuma zake.

https://p.dw.com/p/4g34N
Watu wakikimbia machafuko mashariki mwa Kongo
Mashambulizi ya kila wakati ya kundi la ADF yamekuwa yakisababisha vifo na kuwalazimisha watu kuyakimbia makaazi yako mashariki mwa Kongo. Picha: Nicholas Kajoba/Xinhua/IMAGO

Kamanda huyo, Anywari Al-Iraq, ambaye ni raia wa Uganda, amekamatwa kwenye misitu ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ambako kundi hilo la ADF limekuwa likiendesha operesheni zake.

Taarifa ya jeshi la Uganda imesema kwenye oparesheni iliyofanikisha kukamatwa kwa Al-Iraq huko mkoani Ituri, watu wanane ikiwemo watoto kadhaa wameokolewa. Limesema pia limebaini shehena ya malighafi zinazotumika kutengeneza mabomu ya kienyeji.

Kundi la ADF lenye mafungamano na lile linalojiita Dola la Kiislamu lilianza kama harakati ya uasi nchini Uganda lakini limepiga kambi nchini Kongo tangu mwishoni mwa miaka ya 1990. Linatuhumiwa kufanya mauaji ya mamia ya wanavijiji kwenye uvamizi ambao imekuwa ikifanya miaka ya karibuni.