1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Safari ya kisiasa ya Uganda tangu uhuru

23 Septemba 2025

Siasa za Uganda tangu uhuru 1962 zimegubikwa na mapinduzi, vita na uongozi wa mabavu. Kuanzia Milton Obote, Idi Amin hadi Tito Okello, historia ya taifa imejaa misukosuko na migogoro ya mara kwa mara.

https://p.dw.com/p/50ufu
Uganda Kampala | Mabango ya uchaguzi wa chama tawala NRM
Uganda inajiandaa kwa uchaguzi mkuu mwanzoni mwa 2026 ambao unatarajiwa kurefusha utawala wa muda mrefu wa kiongozi wa taifa hilo Yoweruí Museveni.Picha: Lubega Emmanuel/DW

Uganda ilipata uhuru kutoka Uingereza mwaka 1962. Waziri Mkuu wa kwanza, Milton Obote, alichukua hatamu na baadaye kujitangaza rais. Hata hivyo, siasa za taifa hilo changa zilianza kuyumba mapema kutokana na mgongano wa mamlaka, migawanyiko ya kikabila na tamaa ya viongozi wachanga wa kijeshi.

Mwaka 1971, Jenerali Idi Amin aliongoza mapinduzi yaliyomng'oa Obote. Utawala wake uliendelea kwa miaka minane na kubadilisha taswira ya Uganda kuwa taifa la hofu na ukatili. Mashirika ya kimataifa yaliripoti maelfu ya vifo, mateso na kukimbia kwa raia wengi kwenda uhamishoni.

Amin aliondolewa madarakani mwaka 1979 kupitia operesheni ya kijeshi iliyoongozwa na Tanzania kwa kushirikiana na wapinzani wa Uganda waliohamishwa.

Idi Amin
Idi Amin Dada alimuondoa Militon Obote mwaka 1971 na kuitawala Uganda kwa miaka minane kabla ya kupinduliwa na majeshi ya Tanzania mnano 1979.Picha: AP

Baada ya hapo, Uganda iliingia katika kipindi cha serikali za mpito ambazo hazikudumu. Yusuf Lule, Godfrey Binaisa na Paulo Muwanga waliongoza kwa vipindi vifupi kabla ya Obote kurejea tena madarakani.

Kurejea kwa Obote na mapinduzi mapya

Uchaguzi wa mwaka 1980 ulimrudisha Milton Obote madarakani, lakini mara hii kukiwa na madai makubwa ya wizi wa kura. Kipindi chake cha pili kiligubikwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, maarufu kama "Luwero War,” vilivyochochewa na makundi ya waasi.

Mwaka 1985, Jenerali Tito Okello alimng'oa Obote kupitia mapinduzi. Lakini utawala wa Okello uliendelea kwa miezi sita pekee, kabla ya wapiganaji wa Jeshi la Kitaifa la Ukombozi (NRA) chini ya Yoweri Museveni kuingia Kampala Januari 1986. Hapo ndipo historia mpya ya Uganda ilipoanza kuandikwa.

Kuibuka kwa Museveni

Museveni aliahidi kuleta amani, maridhiano na mabadiliko ya kisiasa. Miaka yake ya awali madarakani ilitafsiriwa na baadhi kama "kipindi cha matumaini mapya,” huku akiahidi kutokomeza siasa za kikabila na kuimarisha uchumi.

Uganda | Rais Yoweri Museveni
Rais Yoweri Museveni ameitawala Uganda kwa mkono wa chuma tangu alipoingia madarakani kupitia vita vya msituni Janauri 1986.Picha: SIMON MAINA/AFP/Getty Images

Mwaka 1996, Uganda ilifanya uchaguzi wa kwanza wa rais kwa kura ya moja kwa moja chini ya katiba mpya. Museveni, akigombea chini ya mfumo wa "Movement,” alishinda kwa zaidi ya asilimia 74. Paul Ssemogerere, mpinzani wake, alitetea demokrasia ya vyama vingi lakini akashindwa vibaya.

Kuibuka kwa Kizza Besigye na demokrasia ya vyama vingi

Mwaka 2001 ulileta changamoto mpya. Daktari Kizza Besigye, aliyewahi kuwa mshirika wa karibu wa Museveni, alijitokeza kumpinga. Kampeni zake zilikumbwa na vitisho na madai ya udanganyifu wa kura. Baada ya kushindwa, Besigye alikimbilia uhamishoni, akiacha kivuli cha upinzani kikikua nchini.

Kauli yake maarufu wakati huo iliibua mijadala: "Huu si uchaguzi wa haki… tumelazimishwa kugombea kama watu binafsi bila msaada wa chama chochote.”

Mwaka 2006, Uganda ilifanya uchaguzi wa vyama vingi kwa mara ya kwanza baada ya miongo miwili. Museveni alishinda kwa asilimia 59, huku Besigye akipata asilimia 37. Lakini kukamatwa kwa Besigye wakati wa kampeni kulichafua taswira ya mchakato huo.

Mwaka 2011, Museveni alishinda tena kwa zaidi ya asilimia 68. Katika hotuba yake ya ushindi, alisisitiza kuwa ushindi huo ulikuwa ushindi wa "itikadi ya mapinduzi dhidi ya siasa za ubaguzi na maslahi binafsi.”

Uganda |  Kizza Besigye | mwanasiasia wa upinzani
Kizza Besigye, aliyewahi kuwa mshirika wa karibu wa Museveni, sasa ni mkosoaji wake mkuu na anashikiliwa gerezani kwa mashtaka ya usaliti ambayo wachambuzi wengi wanayaona kuwa ya kisiasa.Picha: BADRU KATUMBA/AFP

Uchaguzi wa mwaka 2016 ulifanyika kwa mvutano mkali. Baada ya matokeo kutangazwa, Besigye aliapa kama rais katika hafla ya kivuli, hatua iliyomfanya akamatwe na kushtakiwa kwa uhaini. Hata hivyo, Museveni aliapishwa kwa muhula wa tano, akithibitisha udhibiti wake wa kisiasa.

Bobi Wine na wimbi la vijana

Uchaguzi wa mwaka 2021 ulikuwa wa kipekee kutokana na kuibuka kwa Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine. Msanii huyu wa muziki aliyeingia siasa alipata mvuto mkubwa miongoni mwa vijana, akiahidi mageuzi na uwajibikaji. Kampeni zake zilifunikwa na ghasia, vifo na kukamatwa mara kwa mara.

Museveni alitangazwa mshindi kwa asilimia 58, huku Bobi Wine akipata asilimia 35. Wine alikataa matokeo akisema yalikuwa "uchaguzi wenye wizi mkubwa zaidi katika historia ya Uganda.” Nyumba yake iliwekewa mzingiro wa kijeshi na maombi yake ya kupinga matokeo yalitupiliwa mbali na mahakama.

Museveni, kwa upande wake, alisisitiza kuwa huo huenda ulikuwa "uchaguzi huru zaidi dhidi ya wizi tangu 1962.” Kauli yake ilikosolewa ndani na nje ya Uganda, huku nchi za Magharibi zikitoa mashaka kuhusu uhalali wa matokeo.

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda na msanii Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu kama Bobi Wine, akiwa kwenye mkutano wa kisiasa.
Msanii wa muziki aliyeingia kwenye siasa, Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu Bobi Wine (katikati), amekuwa mwiba mkali kwa utawala wa Museveni na sasa anajipanga kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2026.Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Kadri taifa linavyosogea kuelekea uchaguzi wa 2026, Museveni ameonyesha wazi nia ya kugombea tena kupitia chama tawala NRM. Besigye, akiwa amekabiliwa na kesi za uhaini, amebakia nje ya kinyang'anyiro. Bobi Wine ameapa kuendelea kumpinga Museveni licha ya vitisho na ukandamizaji.

Wadadisi wa siasa wanasema kwamba mustakabali wa Uganda unategemea zaidi mshikamano wa upinzani na uaminifu wa wananchi katika taasisi za kikatiba. Wengine wanaonya kuwa bila mageuzi makubwa, taifa linaweza kuendelea kugubikwa na migawanyiko.

Matumaini ya ukurasa mpya

Kwa zaidi ya miaka 60 tangu kupata uhuru, Uganda imepitia vichaka vya misukosuko, mapinduzi, vita na uongozi wa mabavu. Rais Museveni amekuwa sura kuu ya siasa zake,lakini upinzani unaendelea kuonyesha kuwa ndoto ya mabadiliko bado haijazimwa.

Raia wa Uganda sasa wanasubiri kwa shauku mwaka 2026 – uchaguzi ambao unaweza kuamua kama taifa litaendelea na hali ya sasa au kufungua ukurasa mpya wa kisiasa.

Besigye afikishwa mahakama ya kijeshi

Chanzo: Reuters