Museveni kuwa rais wa maisha? | Matukio ya Afrika | DW | 26.02.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Museveni kuwa rais wa maisha?

Wakati upinzani ukiendelea kulalamikia ushindi wa Yoweri Museveni kwenye uchaguzi wa Februari 18, hofu imetanda juu ya uwezekano wa kubadilishwa katiba ili kumuwezesha rais huyo kubaki madarakani maisha yake yote.

Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda.

Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda.

Museveni, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 71, aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 1986, na tangu hapo ametajwa kama mmoja wa viongozi barani Afrika, waliojipendekeza kwa nchi za Magharibi kwa kupambana na ugaidi. Lakini katiba ya sasa inamzuwia kushikilia tena wadhifa huo kwenye uchaguzi ujao, kwa kuwa atakuwa tayari amezidisha miaka 75 inayokubalika kugombea urais.

Upande wa upinzani, wachambuzi na wapiga kura, wanasema walitarajia Museveni angebadilisha kipengele cha umri, kwenye uchaguzi uliofanyika Februari 18, uliompa ushindi wa asilimia 60 ya kura zote. Kwenye uchaguzi huo, chama cha Museveni cha National Resistance Movement (NRM) kilifanikiwa kupata viti 275vya ubunge kati ya 381. Upinzani unapinga matokeo hayo, ukisema yalikuwa ya kughushi, huku NRM ikizitupilia tuhuma hizo.

Wakosoaji wa Museveni wanasema kiongozi huyo mkongwe anafuata njia potofu ya viongozi wa Afrika wanaojaribu kukaa madarakani maisha yao yote, huku wakipuuza wito wa kuzingatia ukomo wa kuwapo madarakani.

Viongozi wengi hukumbwa na woga wa kuachia ngazi, na sababu zake hazielezeki, anasema Nicholas Sengoba, mwandishi wa makala za uchambuzi katika gazeti la Daily Monitor la Uganda.

Kwenye mahojiano ya televisheni yaliyorushwa na shirika la utangazaji la Uingereza, BBC wiki hii, Museveni alionekana kuonyesha wazi uwezekano wa kubadilishwa kwa kipengele cha ukomo wa urais, pale aliposema, "hatuamini katika ukomo wa muhula, kama hamuwataki viongozi kukaa madarakani maisha yao yote, basi msiwapigie kura."

Museveni aliyeongoza vita vya msituni na kumuingiza madarakani katika miaka ya 1980, amekuwa akihusishwa na juhudi za kuleta amani na kuinua uchumi wa Uganda, ingawa bado nchi hiyo inayotazamiwa kuwa mzalishaji mkuba wa mafuta ina changamoto kubwa ya miundombinu duni.

Wakosoaji wanampinga kwa kusema kuwa hakufanya jitihada za kutosha za kuondoa tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana na pia kwenye vita dhidi ya ufisadi. Pia anakosolewa kwa kushindwa kusogeza madaraka kwenye ngazi za chini katika juhudi zake za kuiendeleza Uganda.

Besigye aapa kuendelea kumpinga Museveni

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye.

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye.

Kiongozi wa upinzani, Kizza Besigye, aliyetangazwa kupata asilimia 35 ya kura kwenye uchaguzi wa Februari 18, anamtuhumu Museveni kuuvuruga uchaguzi huo, na ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa alikuwa akitarajia kuwa rais huyo angelifanya njama za kubaki madarakani.

"Iwapo atabadilisha katiba ama la, udikteta kamwe haukubaliki nchini Uganda. Licha ya kampeni yake ya ufidhuli, hatutasimama hadi udikteta utakapoondolewa madarakani," anasema Besigye.

Kwenye baadhi ya mitaa mjini Kampala, wapiga kura wengi wanasema wangeshtushwa kama Museveni angeachia madaraka, ama kwa kutaja jina la atakayempokea ama kustaafu. Zaidi ya robo tatu ya Waganda wapo chini ya miaka 30, na hawajawahi kumjua rais mwingine zaidi ya Museveni.

Kwenye taifa hilo lililowahi kukabiliwa na historia ya muda mrefu ya vurugu chini ya viongozi kama Idi Amini, aliyeendesha serikali iliyojaa ukatili na mauaji ama mateso kwa kiasi cha watu 300,000 katika miaka ya 1970, Museveni anaonekana tafauti na anatajwa kama mdumishaji usalama.

Hata hivyo, aliyewahi kuwa rais wa Marekani, Bill Clinton, alimtaja Museveni kama kiongozi wa kizazi cha sasa cha viongozi wengine wa Afrika wanaoififisha demokrasia. Na sasa, raia wengi wa Uganda wanamfananisha na rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, ambaye mwezi huu ametimiza miaka 92, bila ya kuonyesha dalili za kuachia madaraka.

Mwandishi: Lilian Mtono/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com