1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchunguzi wa Saudi Arabia haukidhi viwango vya kimataifa

24 Agosti 2018

Ripoti mpya yenye kurasa 90 ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch imeeleza kwamba uchunguzi huo kuhusu uhalifu wa vita vya nchini Yemen sio huru na sio wa kuaminika .

https://p.dw.com/p/33iap
Jemen Feuer in Lagerhalle in Hodeida
Picha: Reuters/A. Zeyad

Mkurugenzi wa Human Rights Watch wa Mashariki ya Kati, Sarah Leah Whitson amesema nchi zinazouza silaha kwa Saudi Arabia hazitaepuka kuonekana kuwa zimeshiriki katika vitendo vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Yemen.

Hivi karibuni raia wapatao 31 waliuawa magharibi mwa Yemen katika mashambulio ya makombora huku pande hizo mbili, waasi wa Houthi na umoja wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia unaopambana na waasi hao zikirushiana lawama.

Shirika la habari linaloendeshwa na  waasi la - Saba - limeripoti kuwa wanawake na watoto walikuwa miongoni mwa watu hao waliouawa.  Watu wengine kadhaa walijeruhiwa  baada ya basi walilokuwa wakisafira kushambuliwa na kombora kutoka angani katika wilaya ya Al-Durayhimi, kusini mwa jiji la bandari la Hodeida. Baadhi ya makzi ya watu pia yalishambuliwa.

Mwana mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman
Mwana mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman Picha: picture alliance /dpa/Saudi Press Agency

Wakati huo huo taarifa kutoka nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu, ambayo ni mshirika muhimu katika umoja wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia imesema Wahouthi ndio walioanza kushambulia kwa makombora yaliyotengeenezwa nchini Iran. Kwa mujibu wa shirika la habari la Imarati WAM, Mtoto mmoja aliuawa na wengine kadhaa walijeruhiwa, watoto watatu wakiwa kwenye hali mahututi.

Mfungamano huo wa kijeshi umeshutumiwa kwa kusababisha mateso makubwa kwa watu wa Yemen nchi ambayo inakumbwa na  vita vya wenyewe kwa wenyewe. Nchi hizo zimekubali makossa kwa kiasi kidogo tu, lakini wanarushia mzigo wa lawama waasi wa Houthi kwa kusema kwa kuwatumia raia kama ngao.

Ripoti iliyochapishwa na shirika la Human Rights Watch siku ya Ijumaa imesema uchunguzi wa mfungamano huo juu ya uhalifu wa kivita haukuzingatia uwazi, uadilifu haukuwa huru na ni vigumu kukubalika.

Mtoto aliyetenganishwa na familia yake katiia vita vya nchini Yemen
Mtoto aliyetenganishwa na familia yake katiia vita vya nchini YemenPicha: Reuters/K. Abdullah

Mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch wa Mashariki ya Kati, Sarah Leah Whitson, amesema katika taarifa yake kwamba kwa zaidi ya miaka miwili, ilifahamaila kwamba wachunguzi wa mfungamano huo - JIAT - walikuwa wakifanya uchunguzi wa haki kuhusiana na mashambulio ya anga yanayodaiwa kufanywa   kinyume cha sheria, lakini haikuwa hivyo bali wachunguzi hao walijitahidi tu kufunika ukweli kuhusu uhalifu wa vita.

Mfungamano huo wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umekuwa ukipambana  na waasi wa Houthi wa nchini Yemeni wanaoungwa mkono na Iran tangu mwaka 2015 katika mgogoro mrefu zaidi ambao haujapatiwa ufumbuzi.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE/AFPE

Mhariri: Iddi Ssessanga