Uchaguzi wa Uholanzi wafanyika | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.03.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Uchaguzi wa Uholanzi wafanyika

Waholanzi wapiga kura katika uchaguzi wenye umuhimu mkubwa barani Ulaya kuhusu ushawishi wa vyama vya siasa kali dhidi ya wakimbizi barani Ulaya

Waholanzi leo wanapiga kura ya kuchagua bunge jipya. Uchaguzi huo unatarajiwa kubaini nguvu au ushawishi wa vyama vya siasa kali za kizalendo za mrengo wa kulia barani Ulaya kabla ya chaguzi za Ujerumani na Ufaransa mwaka huu.

Chama cha Waziri Mkuu Mark Rutte VVD ambacho ni cha mrengo wa kulia wa siasa za wastani kinashindana na chama cha ukombozi PVV kinachoongozwa na Geert Wilders miongoni mwa vyama vingine, kila chama kikitaka kuwa na nguvu na ushawishi mkubwa bungeni. Chama cha PVV cha siasa kali kinapinga Uislamu na pia kinaupinga Umoja wa Ulaya.

Wilders wa PVV ndiye anayeonekana kuwa mshindani wa karibu wa waziri mkuu Rutte, hata hivyo nafasi yake ya kushinda ni ndogo ikizingatiwa vyama vyote vimeapa kutoshirikiana naye.

Wapigaji kura katika kituo kimoja cha The Hague

Wapigaji kura katika kituo kimoja cha The Hague

Lakini ushindi wake utazua mshangao barani Ulaya,iwapo utatokea ikizingatiwa ndio uchaguzi wa kwanza mwaka huu katika nchi za Umoja wa Ulaya kabla ya chaguzi za Ujerumani na Ufaransa, ambazo kampeni zao zinatawaliwa na masuala ya siasa kali dhidi ya wakimbizi na uislamu zinazofanana na zinazoendelezwa na Geerts. Geerts anasema haijalishi matokeo ya uchaguzi wa leo, ipo siku dhamira ya chama chake cha ukombozi itatimia.

Wimbi la siasa kali

Waziri Mkuu Mark Rutte ambaye amekaa madarakani  kwa vipindi viwili amesema uchaguzi huo unaonesha  mwendelezo wa ghasia na vurugu, iwapo Wilders atashinda na kueleza kwamba yeye ni mlinzi salama wa Uholanzi na kumrejelea Wilders kama mtu wa siasa kali za mrengo wa kulia asiyetarajiwa kufanya maamuzi magumu akiwa madarakani.

Takriban wapiga kura milioni 13 wanatarajiwa kupiga kura katika vituo vya upigaji kura ambavyo vilifunguliwa tangu alfajiri leo, katika uchaguzi unaotizamwa kuwa jaribio la nguvu za hisia za kizalendo za wanaopinga wakimbizi, hisia ambazo zimetawala katika siku chache zilizopita nchini humo, huku kukiwa na mvutano na Uturuki.

Mvutano wa kidiplomasia kati ya Uholanzi na Uturuki watokota

Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte

Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte

Hapo jana Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alitia mafuta kwenye moto katika mvutano huo alipoonya kulipiza kisasi dhidi ya mauaji ya kimbari ya Srebrenica mwaka 1995 akilaumu majeshi ya kulinda amani ya Uholanzi kutozuia mauaji hayo yaliyofanywa dhidi ya Wabosnia waislamu. Matamshi ambayo yametajwa na Uholanzi kuwa hayana msingi.

Ufaransa inatarajia kumchagua rais wake mpya huku Marine Le Pen wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia akitarajiwa kushiriki duru ya pili ya uchaguzi mwezi Mei. Ujerumani inatarajiwa kufanya uchaguzi wake mwezi Septemba ambapo chama cha siasa kali za mrengo wa kulia AfD ambacho kimekuwa kikimshambulia Kansela Angela Merkel kwa sera yake ya kuwafungulia wakimbizi milango kikitarajiwa kushinda viti vyake vya kwanza katika bunge la chini

Mwandishi: John Juma/RTRE/APE

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com