Tymoschenko kuachiwa huru | NRS-Import | DW | 22.02.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

NRS-Import

Tymoschenko kuachiwa huru

Bunge la Ukraine limeidhinisha kuachiwa huru kwa waziri mkuu wa zamani, Yulia Tymoshenko, kufuatia makubaliano kati ya serikali na upinzani, huku serikali ya Marekani ikitoa wito wa kutekelezwa makubaliano hayo.

Waziri Mkuu wa zamani wa Ukraine, Yulia Tymoschenko.

Waziri Mkuu wa zamani wa Ukraine, Yulia Tymoschenko.

Uamuzi wa kumuachia huru Tymoschenko ambaye amekuwa jela tangu mwaka 2011 unakuja baada ya Rais Viktor Yanukovich na viongozi wa upinzani kutia saini makubaliano yaliyosimamiwa na Umoja wa Ulaya ya kumaliza ghasia ambazo zimeukumba mji mkuu wa nchi hiyo Kiev.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Rais Yanukovich pia amekubali kupunguza nguvu za madaraka ya rais na kufanya uchaguzi wa mapema hapo mwezi Disemba. Kwa upande wake, upinzani utawashawishi waandamanaji wanaomtaka Yanukovich aondoke madarakani kuondoka kutoka Uwanja wa Uhuru ambao wameukalia kwa miezi mitatu sasa.

Marekani yataka makubaliano yatekelezwe

Rais Barack Obama wa Marekani (kulia) na Rais Vladimir Putin wa Urusi walipokutana mwezi Septemba 2013, St. Petersburg, Urusi.

Rais Barack Obama wa Marekani (kulia) na Rais Vladimir Putin wa Urusi walipokutana mwezi Septemba 2013, St. Petersburg, Urusi.

Serikali ya Marekani imetoa wito wa kutekelezwa kikamilifu kwa makubaliano hayo, huku ikionya kuwa inaweza kuwa vigumu kuwashawishi waandamanaji wenye msimamo mkali kuweka chini silaha zao.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jan Carney, alisema makubaliano hayo yanayoirejesha katiba ya awali inayopunguza madaraka ya rais yanalingana na kile ambacho Marekani ilikuwa inakipigania, lakini akaongeza kwamba nchi hiyo itafuatilia kwa karibu ikiwa kweli kuna hatua madhubuti za utekelezaji.

Utawala wa Rais Barack Obama umekuwa ukifikiria kuwawekea vikwazo maafisa wa serikali ya Ukraine wanaohusika na kuchochea ghasia, lakini Carney aliashiria kwamba hatua hiyo itasitishwa kwanza huku serikali ikifuatilia utekelezaji wa makubaliano hayo ya Ijumaa.

"Mtazamo wetu ni kushirikiana na wenzetu wa Ulaya na pia serikali na upinzani nchini Ukraine kuhakikisha kwamba makubaliano hayo yanatekelezwa," alisema Carney, akiongeza kwamba bado uwezekano wa vikwazo haujaondoshwa.

Obama azungumza na Putin

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov (kushoto) akizungumza na mwenzake wa Marekani, John Kerry, walipokutana mjini Washington, mwezi Agosti 2013.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov (kushoto) akizungumza na mwenzake wa Marekani, John Kerry, walipokutana mjini Washington, mwezi Agosti 2013.

Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Marekani, ambaye anafuatilia kwa karibu machafuko ya Ukraine, amesema hali ya mashaka iliyokuwapo kati ya Marekani na Urusi juu ya mzozo wa Ukraine imepungua, akitaja mazungumzo ya muda wa zaidi ya saa moja kwa njia ya simu kati ya Rais Barack Obama na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, kwamba yalikuwa na ufanisi.

Kwa mujibu wa afisa huyo ambaye hakuruhusiwa kutajwa jina, mazungumzo ya viongozi hao wawili yalihusu namna ambavyo makubaliano ya serikali na upinzani nchini Ukraine yatakavyoleta utulivu, kumaliza ghasia na kupelekea kupatikana kwa amani. Urusi imesema inataka kuwa sehemu ya utekelezaji wa makubaliano hayo.

"Makubaliano haya ni dhamira kwamba Ukraine imejinasua kutoka kwenye ukingo wa machafuko na kwamba pande zote zinahitaji kusaidia kufikiwa kwa umoja wa kisiasa na kuurudisha uchumi wa taifa hilo kwenye hali nzuri," alisema afisa huyo, ambaye pia aliongeza kuwa katika mazungumzo hayo Rais Putin hakulalamikia kuwa Marekani inaingilia mambo ya ndani ya Ukraine, kauli ambayo mara kwa mara hutolewa na maafisa waandamizi wa serikali yake.

Kujihusisha kwa Marekani

Rais Viktor Yanukovych akizungumza na ujumbe wa Umoja wa Ulaya mjini Kiev, tarehe 20 Februari 2014.

Rais Viktor Yanukovych akizungumza na ujumbe wa Umoja wa Ulaya mjini Kiev, tarehe 20 Februari 2014.

Mazungumzo mengine kwa njia ya simu yalifanywa kati ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Chuck Hagel, na mwenzake wa Ukraine, Pavlo Lebedev, ambapo Lebedev alimuambia Hagel kuwa jeshi la Ukraine halitotumia silaha dhidi ya watu wake na kwamba wanajeshi wamewekwa tu kulinda vituo vya kijeshi.

Kwa upande wake, Hagel alisifia hatua ya Ukraine kulitenga jeshi na mgogoro uliopo. Wizara ya Ulinzi ya Marekani imesema kwamba kabla ya mazungumzo ya hapo Ijumaa kati ya mawaziri hao wawili, Hagel alijaribu mara kadhaa kumpigia simu Lebedev lakini zilikuwa hazipokewi.

Vile vile, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry alizungumza na viongozi watatu wakuu wa upinzani siku hiyo hiyo ya Ijumaa aliowaeleza kuwa Marekani inaendelea kuunga mkono jitihada za amani, na naibu wake wa masuala ya Ulaya, Victoria Nuland, alizungumza na waziri wa mambo ya nje wa Ukraine.

Siku ya Alhamisi, Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden, alifanya mazungumzo ya saa nzima kwa njia ya simu na Rais Viktor Yanukovich, ikiwa ni mara ya tisa kufanya hivyo tangu mwezi Novemba.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, William Burns, anatarajiwa kuwasili mjini Kiev wiki ijayo na Nuland amepangiwa kuwapo Ukraine mapema mwezi Machi, kwa mujibu wa maafisa wa Marekani.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Caro Robi

DW inapendekeza

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com