1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Twaweza yaandamwa na serikali Tanzania

Sylvia Mwehozi
3 Agosti 2018

Shirika la utafiti la Twaweza Tanzania limedai kwamba linapitia kipindi kigumu baina yake na baadhi ya taasisi za kiserikali kufuatia uzinduzi wa taarifa za ripoti zake mbili hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/32bDG
Tansania | Aidan Eyakuze
Picha: DW/S. Khamis

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari shirika hilo limesema Idara ya Uhamiaji imeishikilia pasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza ya kusafiria tangu Julai 24, hatua inayokuja baada ya kuchapisha tafiti zake za Sauti za Wananchi mnamo Julai 5 zenye vichwa vya habari "Kuwapasha Viongozi?" na "Nahodha wa Meli yetu Wenyewe?"

Taarifa hiyo inasema siku ya Agosti 1, mkurugenzi wake Aidan Eyakuze alizuiliwa kusafiri kwa kutumia pasi ya dharura iliyotolewa kwa utaratibu uliopo, ili aweze kushiriki mikutano ya kikazi kwenye ofisi za Twaweza kwenye miji ya Nairobi, Kenya, na Kampala, Uganda. 

Akizungumza DW, msemaji wa idara ya uhamiaji ya Tanzania, Ali Mtanda, alikiri kuwa idara yake inaishikilia pasi ya kusafiria kwa kile alichosema ni "uchunguzi wa uraia wake."

Mtanda alisema idara hiyo ilipokea taarifa za utata kuhusiana na uraia wa mkurugenzi huyo wa Twaweza na kwa hivyo wanatimiza taratibu zao.

Tansania Präsident John Magufuli
Rais wa Tanzania John Magufuli Picha: DW/S. Khamis

Alipoulizwa ikiwa hatua hiyo inalenga kulinyamazisha shirika la Twaweza kutokana na tafiti zake zilizotolewa hivi karibuni, Mtanda alitupilia madai hayo akisema "hayana ukweli na yanapaswa kupuuzwa."

Mwenyewe Eyakuze katika mazungumzo kwa njia ya simu na DW, alisema hakuwa ameelezwa sababu za uraia wake kutiliwa shaka na mamlaka za nchi.

"Nimezaliwa Tanzania, kiasilia wazazi wangu wamezaliwa Tanzania, kwa uelewa wangu kwa sheria za Tanzania, uraia wangu ni halali", alisema Eyakuze.

Twaweza pia ilikiri kupokea barua mbili kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambazo zinahoji uhalali wa programu ya Sauti za Wananchi na kuwataka watoe ufafanuzi kwa nini hatua za kisheria zisichukuliwe dhidi yao.

Utafiti wa hivi karibuni wa Twaweza uliobainisha matokeo mbalimbali yakiwemo yale ya kushuka kwa umaarufu wa Rais John Magufuli ulizua mawazo mchanganyiko katika mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari.

Matokeo ya tafiti hizo pia yalianisha kupungua kwa uhuru wa vyama vya upinzani, asasi za kiraia na vyombo vya habari.

Mhariri: Sylvia Mwehozi
Mhariri: Mohammed Khelef