Tsvangirai ampa saa 24 Mugabe | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 26.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Tsvangirai ampa saa 24 Mugabe

Viongozi wa Zimbabwe watakiwa wawajibike

Morgan Tsvangirai akizungumza na waandishi habari mjini Harare

Morgan Tsvangirai akizungumza na waandishi habari mjini Harare


Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai amelisihi bara la Afrika liingilie kati katika mzozo wa nchi yake,akimpa wakati huo huo rais Robert Mugabe muda wa saa 24 akubali kujadiliana.Katika mahojiano pamoja na gazeti la Uengereza "Times",kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC,Morgan Tsvangirai, aliyeamua kususia duru ya pili ya uchaguzi wa rais, amesema halitozuka tena suala la kujadiliana pamoja na Mugabe ikiwa uchaguzi utafanyika kama ilivyopangwa hapo kesho.


Morgan Tsvangirai anamtaja rais Mugabe kua "ni kiongozi haramu" ."Hakutakua tena na majadiliano ikiwa Mugabe atajitangaza mshindi na kuendelea kujiiita rais,"amesema hayo kiongozi huyo wa upinzani aliyekimbilia katika ubalozi wa Uholanzi tangu jumapili iliyopita.


Morgan Tsvangirai anamtuhumu rais Mugabe kua nyuma ya visa vya matumizi ya nguvu yaliyogharimu maisha ya raia kadhaa wasiokua na hatia.


"Anaesakwa hasa ni mie" amesema kiongozi huyo wa MDC akijibu suala lini anapanga kuuhama ubalozi wa Uholanzi.


Morgen Tsvangirai aliyemaaloza wa kwanza katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais amewatolea mwito viongozi wa Umoja wa Afrika na jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC wabuni mkakati wa muda utakaoiauni nchi yake,na kutoa mwito pia watumwe wanajeshi wa kulinda amani nchini humo.Morgen Tsvangirai anasema:


"Daima tumekua tukisema kwamba tatizo la Zimbabwe linabidi lifumbuliwe na bara la Afrika.Kwa hivyo nnautaka Umoja wa Afrika na jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC kwa pamoja,wasimamie mpango ulioshauriwa na Umoja wa mataifa wa kubuniwa kipindi cha mpito.Tunashauri tume ya suluhu ya Umoja wa Afrika,inayowajumuisha viongozi mashuhuri,ibuni kipindi cha mpito kitakachotilia maanani matakwa ya wananchi wa Zimbabwe,kama walivyotamka March 29 iliyopita."


Mzozo wa Zimbabwe unatazamiwa kugubika mkutano wa viongozi 53 wa umoja wa Afrika watakaokutana kuanzia june 30 hadi July mosi huko Charm El Sheikh nchini Misri.


Kwa upande wa kimkoa,Zimbabwe iligubika mkutano wa dharura ulioitishwa jana na kamisheni ya usalama ya jumuia ya ushirikiano kusini mwa Afrika SADC mjini Mbabane nchini Swaziland.


Mwishoni mwa majadiliano hayo,mfalme Mswati wa Swaziland,rais Jakaya Kikwete wa Tanzania ambae ndie mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Angola Joao Miranda wametoa mwito "uchaguzi wa Zimbabwe uakhirishwe ."


Hata rais mstaafu wa Afrika kusini Mzee Nelson Mandela ameamua kupaza sauti na kukosoa kile anachokiita "uzembe mkubwa" wa viongozi wa Zimbabwe.


Kwa upande wake waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice akiwa ziarani nchini Japan kuhudhuria mkutano wa mataifa tajiri kiviwanda G8, amewasihi viongozi wa Zimbabwe wafikie makubaliano haraka iwezekanavyo kwa kutilia maanani matokeo ya chaguzi zilizotangulia.


Wakati huo huo watu 200,wake kwa waume na watoto,wanaodai kua wahanga wa matumizi ya nguvu nchini Zimbabwe, wamekimbilia katika ubalozi wa Afrika kusini mjini Harare jana usiku.


►◄
 • Tarehe 26.06.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/ERG6
 • Tarehe 26.06.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/ERG6
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com