1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aonya kuiteketeza Iran kama haitafikia makubaliano

18 Mei 2026

Rais wa Marekani Donald Trump kwa mara nyingine tena ametishia kuiteketeza Iran, wakati akiendelea kuishinikiza Tehran kukubaliana na mpango wa kumaliza vita.

https://p.dw.com/p/5Dt9Y
Rais Donald Trump akirejea Marekani kutoka ziarani China
Trump ameelezea mara kwa mara kukerwa kwake na ukosefu wa maendeleo katika mahusiano na IranPicha: Jacquelyn Martin/AP Photo/dpa/picture alliance

Trump amesema muda unayoyoma kwa Iran na kwa hiyo wanapaswa kuchukua hatua ya haraka lasivyo hakuna kitakachobaki nchini humo. Makubaliano ya kusitisha vita yalifikiwa mapema Aprili, ambayo Trump hivi karibuni aliyarefusha, lakini hakuna makubaliano ya kudumu yaliyofikiwa na Iran.

Wiki iliyopita, rais huyo wa Marekani alisema mpango wa usitishaji mapigano unakaribia kuvunjika. Hapo jana, vyombo vya habari vya Iran vilisema Marekani imeshindwa kufanya makubaliano yoyote halisi katika jibu lake la hivi karibuni kwa ajenda iliyopendekezwa na Iran ya mazungumzo ya kukomesha vita.

Shirika la habari la Fars lilisema Washington imewasilisha orodha ya vipengele vitano ambayo inajumuisha sharti la kuitaka Iran kubaki na kiwanda kimoja tu cha nyuklia kinachofanya kazi na kuihamishia Marekani hifadhi yake ya urani iliyorutubishwa.

Matumaini hafifu

Matumaini ya kufanikisha mpango huo wa amani yanaonekana kukwama kutokana na mivutano na mashambulizi madogo ya kila upande.  Spika wa Bunge la Iran Mohammad Bagher Ghalibaf amesema mzozo huo unayumbisha usalama wa Mashariki ya Kati na kwamba uwepo wa Marekani eneo hilo umechangia pakubwa katika kuzorota kwa hali hiyo.

Washington na Tehran zimekuwa zikijadiliana kwa kutuma mapendekezo kupitia mpatanishi Pakistan, lakini hadi sasa zimeshindwa kufikia makubaliano ya kudumu ya amani huku pande zote zikituhumiana kwa kuwa na masharti magumu na yasiyotekelezeka.