1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yaomboleza, ajali ya MV Nyerere yauwa watu 86

Daniel Gakuba
21 Septemba 2018

Shughuli za uokozi zimeanza tena kuwatafuta wahanga wa ajali feri ya MV Nyerere ambayo ilipinduka Alhamis katika Ziwa Victoria, Tanzania. Watu 37 waliokolewa wakiwa hai. Rais Magufuli amepeleka salamu za rambirambi.

https://p.dw.com/p/35HLY
Tansania Fährunglück | MV Nyerere vor dem Unglück
MV Nyerere kabla ya kupata ajaliPicha: Zadock of SAUT, Mwanza

Idadi ya watu ambao wamefariki dunia nchini Tanzania kutokana na ajali ya kivuko cha MV Nyerere kilichopinduka jana Alhamis katika Ziwa Victoria, imeongezeka na kufikia watu 86. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti kwenye gazeti la kibinafsi nchini humo Citizen. Hapo awali kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali nchini humo kiliripoti kuwa idadi ya vifo iliongezeka hadi 79, kikimnukuu mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella. Hadi jioni ya jana, waokozi walikuwa wameweza kuwapata watu 37 wakiwa hai, haya yakiwa ni kwa mujibu wa mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mogella. Kulingana na taarifa za maafisa wa Tanzania, idadi ya vifo inatazamiwa kuongezeka na juhudi za uokozi zinaendelea.

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, na kuwatakia nafuu ya haraka waliojeruhiwa. Wakala wa Ufundi na Umeme unaohusika kusimamia chombo hicho umewataka wananchi kuwa na subira katika taarifa yake huku juhudi za uokozi zikiwa zimeshaanza.

Kupakia kupita uwezo

Shirika hilo limesema kivuko hicho kilikuwa kinatoka Ukara na kuelekea Bugolora  na kilizama karibu na Mwanza. Mwandishi wa DW aliyeko Mwanza, akimnukuu mkuu wa wilaya ya Ukerewe Colnel Magembe, amesema kivuko kilichopata ajali kilikuwa kikibeba abiria zaidi ya uwezo wake, kwa sababu ingawa kinatakiwa kupakia wasiozidi 100, kilipopata ajali kilikuwa kimejaza abiria zaidi ya 300.

Tansania Fährunglück Viktoriasee
Wananchi wakifuatilia kwa huzuni shughuli za uokoziPicha: Zadock of SAUT, Mwanza

Amesema wakati kivuko hicho kikikaribia kwenye bandari ndogo ya Bwisa, watu wengi walitaka kushuka kwa wakati mmoja, wakajazana mbele na kusababisha uzito wote sehemu moja, na hivyo kusababisha kuzama.

Hali hiyo ya msongamano katika kivuko hicho, amesema Bulendu, hujitokeza hasa siku ya Alhamis kwa sababu ya mnada unaofanyika siku hiyo kwenye soko la Bwisa kisiwani Ukara.

Matukio ya mara kwa mara

Ajali za vyombo vya majini ni tukio la mara kwa mara katika maziwa ya Tanzania na Uganda, mara nyingi zikitokana na uchakavu wa vyombo hivyo, au kupakia abiria na mizigo kupita uwezo.

Mwaka 1996, ajali mbaya zaidi iliyohusisha meli ya MV Bukoba iliuwa watu wasiopungua 800 katika ziwa hilo la Victoria.

Mwaka 2011, ajali nyingine mbaya ya meli ya MV Spice Islander ilizama katika Bahari ya Hindi karibu na pwani ya Zanzibar, na kuuwa watu zaidi ya 200.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape, afpe, dw

Mhariri: Buwayhid, Yusra