Tanzania: Ukandamizaji ulihujumu uchaguzi | Matukio ya Afrika | DW | 23.11.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Tanzania: Ukandamizaji ulihujumu uchaguzi

Serikali ya Tanzania ilihusika na mauaji ya watu wanne na matendo mengine ya ukandamizaji yaliyoathiri uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020, limesema Jumatatu shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch.

Shirika la Human Rights Watch linaitaka serikali ya Tanzania kuchunguza dhuluma hizo, na kusitisha unyanyasaji wa waandishi wa habari na wanasiasa wa upande wa upinzani, pamoja na kuondoa vizuizi vilivyowekewa vyombo vya habari siku chache kabla ya siku ya uchaguzi.

Baada ya kampeni za uchaguzi kuanza mnamo mwezi Agosti, polisi waliwakamata viongozi kadhaa wa vyama vya upinzani pamoja na wafuasi wao.

Soma zaidi: Polisi Tanzania yawashikilia viongozi wa upinzani

Katika wiki zilizofuatia uchaguzi, serikali ilisitisha kwa muda matangazo ya baadhi ya vituo vya televisheni na redio, ilifuatiliwa mawasiliano ya watu ya njia ya simu, pamoja na kuzuia mawasiliano ya mitandao ya kijamii.

Usiku wa kuamkia siku ya uchaguzi, polisi walifyatua risasi za moto dhidi ya umati wa watu katika visiwa vya Zanzibar, vyenye mamlaka ya ndani, na kuua watu wasiopungua watatu.

"Ukandamizaji uliofanywa na serikali ya Tanzania dhidi ya upinzani na vyombo vya habari wakati wa kampeni za uchaguzi ulihujumu kampeni hizo," amesema Oryem Nyeko, mtafiti wa masuala ya Afrika katika shirika la Human Rights Watch amesema. "Serikali ya Tanzania inapaswa kuchunguza ukiukaji huu wa haki za binadamu uliotendwa wakati wa uchaguzi na kuachana na tabia za kutumia matendo ya unyanyasaji."

Magufuli ashinda ushindi wa kishindo

Rais John Pombe Magufuli  wa chama tawala wa CCM, alitangazwa mshindi kufuatia uchaguzi huo wa Oktoba 28. Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi ilimtangaza kupata asilimia 84 ya kura zote zilizopigwa, na kumshinda mpinzani wake mkuu wa chama cha Chadema, Tundu Lissu.

Shirika la Human Rights Watch lilifanya mahojiano ya simu na watu 16 kutoka Oktoba 15 hadi Novemba 9, ikiwa ni pamoja na waandishi habari, vongozi wa vyama vya kisiasa, pamoja na wanafamilia wa watu wanaodaiwa kuuliwa na polisi.

Tazama vidio 03:29

Athari za kusuasua kwa huduma za Intaneti Tanzania

Shirika hilo la kimataifa limeorodhesha kukamatwa kwa maafisa wasiopungua 18 wa vyama vya upinzani, pamoja na wafuasi wao. Miongoni mwao ni Lissu na mgombea mwingine wa urais, Seif Sharif Hamad wa chama cha ACT Wazalendo, kabla na baada ya uchaguzi. Chama cha Chadema kiliripoti kuwa wanachama wake wapatao 300 walikamatwa kote nchini Tanzania katika kipindi hicho cha kabla na baada ya uchaguzi.

Human Rights Watch limesema vitendo vilivyofanywa na serikali ya Tanzania wakati wa uchaguzi vimeonyesha dhahiri kwamba imeshindwa kuheshimu haki za msingi za wananchi ikiwa ni pamoja na kuwa na uhuru wa kujieleza, pamoja na kufanya mikutano na maandamano kwa njia za amani na hilo linatia wasiwasi.

"Sikali ya rais Magufuli inapaswa kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha haki za binadamu zinaheshimiwa wakati wote nchini humo." ameeleza Nyeko.

Chanzo: HRW