1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania na mapenzi ya jinsia moja: Taswira na uhalisia

18 Novemba 2018

Kama kuna jambo limeangaziwa sana kilimwengu nchini Tanzania katika siku za hivi karibuni, basi ni kampeni ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, dhidi ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, ambapo ukosoaji kutoka jumuiya ya kimataifa na wanaharakati unatajwa kuwa mkubwa zaidi kuliko ilivyowahi kushuhudiwa kwenye matukio mengine.

https://p.dw.com/p/38Ri7

Matamko ya kulaani hatua hiyo yamekuwa makali na wakati mwengine hatua za kujibu hatua hiyo pia zimekuwa kubwa, kama ile ya kutishia au kuzuia misaada na mikopo kutoka mataifa wahisani au taasisi za fedha za kimataifa. 

Katika dunia ya sasa, suala la haki za binaadamu linahusisha binaadamu wote, bila kujali jinsia au muelekeo wao wa kijinsia na mahusiano ya kimapenzi. Hapa ndipo suala hili linapojadiliwa kwa mtazamo wa haki za binaadamu. 

Lakini dunia ya leo pia huongozwa kwa sheria na kanuni, na bila kusahau misingi ambayo jamii fulani imejiwekea kama mila, desturi na utamaduni wake. Hapa ndipo suala hili linapojadiliwa kwa mtazamo wa tafauti baina ya jamii na jamii. 

Je, kwa hayo yote, matamko yanayotolewa na viongozi wa Tanzania - kama hili la kampeni dhidi ya wapenzi wa jinsia moja - yanaiweka wapi taswira ya taifa hilo la Afrika Mashariki kilimwengu?

Na kwa upande wa pili, hatua kama hizi zinazochukuliwa na jumuiya ya kimataifa dhidi ya Tanzania, zinawaweka nafasi gani watu wale wale ambao wanaochukuwa hatua hizo wanasema wanataka kuwalinda?

Juu ya yote, u wapi mstari baina ya dhana hizi tatu: haki za binaadamu, sheria na maadili ya kijamii?

Mada mbele ya Meza ya Duara leo ni "Tanzania na Wapenzi wa Jinsia Moja: Mtazamo, Muelekeo na Uhalisia!" Muongozaji ni Mohammed Khelef na washiriki ni Sweetbert Nkuba, mwanasheria kutoka Tabora, Tanzania; Jabir Idrissa, mwandishi wa habari na mchambuzi akiwa Zanzibar; Fatma Karume, wakili wa kujitegemea na mwanaharakati wa haki za binaadamu; na Abu (sio jina lake halisi), ambaye mwenyewe ni mtu anayeshiriki mapenzi ya jinsia moja kutoka Tanzania.