1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania imekabidhi baraza la mawazi la SADC kwa Msumbiji

13 Agosti 2020

Tanzania imekabidhi uenyekiti wa baraza la mawaziri wa nchi za jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika SADC kwa Msumbuji, huku ikikiri janga la virusi vya Corona lilikuwa changamoto kubwa miongoni mwa nchi wananchama.

https://p.dw.com/p/3gutV
Tansania SADC Ministertreffen Videokonferenz
Picha: Office of the Prime Minister of Tanzani

Licha ya janga hilo lakini, Tanzania imesema yalipatikana mafanikio kadhaa. Katika mkutano wa arobaini tangu jumuiya hiyo kuundwa ikiwa ni utaratibu wa kawaida kupishana katika kiti, sasa ni zamu ya Msumbiji kushika hatamu ya jumuiya hiyo kongwe iliyo kusini mwa Afrika.

Mapema leo katika mkutano wa baraza la mawaziri SADC lililofanyika kwa njia ya mtandao, waziri wa mambo ya nje nchini Tanzania Profesa Paramagamba Kabudi amemkabidhi balozi wa Msumbiji uenyekiti kwa niaba ya taifa lake, huku akisisitiza kuwa mbali na changamoto ya janga la virusi vya Corona wamefanikiwa masuala kadhaa ikiwemo kuimarisha hali ya amani na usalama pamoja na kukuza democrasia ambayo ilishuhudiwa katika mataifa kadhaa ikiwemo Malawi kufanyika uchaguzi huru na haki.

Majanga ambayo SADC imekabiliana nayo.

Filipe Nyusi, Präsident von Mosambik (D. Anacleto)
Rais Filipe Nyusi wa MsumbijiPicha: DW

Aidha mbali na ya virusi vya corona majanga ya asili ikiwemo kimbunga Kenneth yanatajwa kuwa ni sehemu ya changamoto ilioikumba jumuia, ambapo kwa pamoja waliungana katika kuhakikisha watu wanapata huduma za kibinadamu kwa wakati huku wakiendelea kusaka suluhu ya kudumu.

Itakumbukwa kuwa Tanzania imekuwa mwenyekiti wa jumuiya tangu mwezi Agosti mwaka uliopita ambapo leo inakabidhi baraza hilo la mawaziri ikiwa bado haijafanikisha kupitisha ajenda ya maendeleo kwa kipindi cha miaka 10 wakati ile ya 2010-2020 ikikamilika kwa mafanikio. Ajenda ambayo itakuwa miongoni mwa zoezi ambalo Msumbiji italazimika kuipitisha.

Punde baada ya kupokea bendera ya SADC pamoja na zana zingine za kiutendaji balozi wa Msumbiji nchini Tanzania Monica Mussa amesema, wamepokea jukumu la kuendeleza maendeleo ya jumuia ili kufikia malengo yake, ikiwemo kukabiliana na umasikini, kukuza na kuendeleza democrasia pamoja na kuendeleza uchumi wa viwanda.

Soma zaidi:SADC yatakiwa kukemea ukandamizaji Zimbabwe

Mnamo Agosti 17 2020 wakuu wa nchi wa jumuiya hiyo watakutana, ambapo mbali na ajenda nyingine Rais John Magufuli wa Tanzania atakabidhi uenyekiti wa SADC kwa Rais wa Msumbiji Philipe Nyusi huku akibeba kauli mbiu, SADC miaka 40 ya kuimarisha amani na usalama na kuhimili changamoto zinazoikabili dunia.