1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sokwe wanakabiliwa na kitisho cha kutoweka

Josephat Nyiro Charo12 Agosti 2014

Familia kubwa ya sokwe ulimwenguni inakabiliwa na kitisho cha kuangamia katika miongo kadhaa ijayo. Onyo hilo limetolewa na mtalaamu maarufu wa sokwe, Jane Goodall.

https://p.dw.com/p/1CsbK
Primatenforscherin Jane Goodall mit Schimpansen
Picha: AP

Jane Goodall ametoa wito kwa wahusika kuhakikisha kuwa wanyama hao walio na ukoo wa karibu na mwanadamu hawaangamii kabisa. Akizungumza mjini Nairobi, Bi Goodall amesema kama hatutachukua hatua sasa, masokwe wataangamia, kwa sababu ya uharibifu wa makazi yao pamoja na biashara ya usafirishaji haramu.

Goodall ambaye ni mwanasayansi wa Uingereza ambaye ametumia miongo mitano iliyopita akifanya utafiti kuhusu sokwe katika Mbuga ya Kitaifa ya Gombe nchini Tanzania anasema katika nusu karne iliyopita, idadi ya sokwe imepungua kutoka takribani milioni mbili hadi kufikia laki tatu pekee, katika nchi 21. Anasema kama hapatakuwa na mabadiliko yoyote, bila shaka sokwe watatoweka, au kuwachwa katika maeneo machache sana ambako watasumbuka kutokana na uzalishaji.

Watalaamu wanabashiri kuwa katika kiwango cha sasa, maendeleo ya binadamu yataathiri asilimia 90 ya makazi ya sokwe barani Afrika na asilimia 99 barani Asia ifikapo mwaka wa 2013, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa mwezi uliopita na kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

04.09.2009 DW-TV PROJEKT ZUKUNFT Schimpanse
Sokwe wako hatarini kuangamiaPicha: DW-TV

Maendeleo ya miundo mbinu na matumizi ya mali asili – ikiwa ni pamoja na mbao, madini, mafuta na gesi – yameathiri kabisa makazi ya sokwe na kuifanya familia ya wanyama hao kuwa katika kitisho kikubwa cha kuangamia.

Uharibifu unafanywa na binadamu

Kwake Goodall, uharibifu huu ni sehemu ya shambulizi linalofanywa na mwanadamu dhidi ya mazingira. Anasema kama hatutafanya chochote kuyatunza na kuyalinda mazingira, ambayo tayari tumeyaharibu kwa kiwango Fulani, asingetaka kuwa mtoto atakayezaliwa katika kipindi cha miaka 50 ijayo.

Mtaalaamu huyo anaongeza kuwa kifo cha sokwe, ambao ni jamaa za karibu kabisa na mwanadamu, kinaweza kutumika kama onyo kali la mabadiliko ya tabia nchi na ongezeko la joto duniani. Kwa sababu kama wanyama hao wataangamia, itakuwa na maana kuwa tumeipoteza misitu yetu, na hilo litakuwa na athari kubwa zaidi kwa mabadiliko ya tabia nchi. Anasema kuna viongozi ambao wanasema hawataki kuamini kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, lakini yeye hawezi kuamini kuwa viongozi hao kweli wanaamini hilo, labda kwa sababu ni wapumbavu tu.

Goodall, ambaye ameunda makundi ya uhifadhi barani Afrika, anatoa wito kwa watu kutokata tama na badala yake kuchukua hatua. Anasema mabadiliko ya tabia nchi yanatishia kila sehemu ya dunia, na hatuwezi kuzuia hilo, lakini kama tutaungana pamoja tunaweza kupunguza athari zake.

Mtafiti huyo anasema ujumbe wake kwa kila mtu ni kufahamu kuwa maisha yako yana umuhimu, na maisha yako yanaweza kuleta mabadiliko. Hivyo ni wakati wa kuchukua hatua hata kama ni hatua ndogo tu, ili kusaidia kuyalinda maisha ya sokwe.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo