1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Tanzania yatoa ripoti ya ajali ya ndege

25 Novemba 2022

Serikali ya Tanzania imetoa ripoti ya ajali ya ndege ya Precision iliyoanguka Novemba 6, katika Ziwa Victoria, huku ikikumbwa na maswali mengi kutokana na hatua yake ya awali kuikana ripoti iliyovuja.

https://p.dw.com/p/4K2kL
Tansania | Flugzeugabsturz in den Victoriasee
Picha: REUTERS

Ripoti hiyo ya awali iliyotolewa na waziri wa uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa inafanana kabisa na ripoti ya awali iliyochapishwa na vyombo vya habari na katika mitandao mingine ya kijami ambayo ilibainisha kuwepo kwa uzembe wakati wa uokoaji wa abiria waliokuwepo kwenye ndege hiyo aina ya ATR.

Kwa ujumla ripoti ya serikali imebainisha hali yote yaliyohusisha ajali hiyo kuanzia mazingira ya ajali yenyewe mpaka hatua za uokoaji, mambo ambayo pia yamejitokeza katika ripoti ya awali iliyoibuliwa na vyombo vya habari.

Kabwe: Serikali iombe msamaha kuhusu vifo vya ajali ya ndege

Katika ripoti yake, Waziri Mbarawa ameeleza namna mabadiliko ya hali ya hewa katika uwanja wa ndege wa Bukoba ilivyobadilika hali iliyomfanya rubani wa ndege hiyo kutumia muda mwingu kuzunguka hewani  kabla ya kuchukua uamuzi wa kutua na hatimaye kusababisha ajali hiyo.Lakini, kijana anayefahamika kwa jina la Majaliwa ambaye anaelezwa ndiye shujaa aliyefungua mlango wa ndege na kuendesha uokoaji hajatajwa katika ripoti ya serikali na hata ile iliyovuja licha ya kupewa sifa kemu kemu ikiwamo kukaribishwa bungeni na kupungezwa.Chanzo cha ajali ya ndege iliyouwa watu 19 hakijajulikana

Baadhi ya majeneza ya walioangamia kwenye ajali ya ndege katika ziwa Victoria nchini Tanzania Novemba 6, 2022.
Baadhi ya majeneza ya walioangamia kwenye ajali ya ndege katika ziwa Victoria nchini Tanzania Novemba 6, 2022.Picha: SITIDE PROTASE/AFP

Hatua ya serikali kutangaza ripoti yake ikiwa siku moja tu baada ya msemaji wake, Greyson Msigwa kuikana ripoti iliyovuja kwa vyombo vya habari, imezusha mjadala mkubwa  na wengine wakihoji namna serikali hiyo inavyoshughulikia mambo yake hasa katika nyakati hizi za ulimwengu wa kidigitali.

Wachambuzi wa mambo wanasema kwa namna yoyote ile, serikali  ilipaswa kulitazama jambo hilo kwa umakini tena kwa tahadhari kubwa baada ya ripoti hiyo kuvuja kwa vyombo vya habari.

Wakosoaji wengi wamesema lau serikali ingewajibika zaidi, basi vifo vingi vingeepushwa.
Wakosoaji wengi wamesema lau serikali ingewajibika zaidi, basi vifo vingi vingeepushwa.Picha: SITIDE PROTASE/AFP

Mwanahabari wa siku nyingi na mhariri, Abdulsalamo Kibanda anasema Serikali ilikuwa haina sababu ya kuikana ripoti hiyo baada ya kubaini imevuja kwa vyombo vya habari.

Tarehe 6 mwezi huu wa Novemba, ndege ya shirika la Precision ilianguka katika Ziwa Victoria wakati ikijiandaa kutua katika uwanja wa ndege wa Bukoba, ikiwa safarini kuelekea Mwanza ikitoea jijini Dar es Salaam.

 Watu 19 walipoteza maisha wakiwamo pia raia kadhaa wa kigeni. Wataalamu kutoka Ufaransa ambako ndiko ndege hiyo ilikotengenezwa, nao pia wamekuwa wakiendesha uchunguzi wao kuhusiana na ajali hiyo na ripoti yao bado haijatolewa.