Rwanda yaikosoa DRC kwa kukataa kusaini mkataba wa biashara
6 Oktoba 2025
Rwanda imesema mkataba huo chini ya uratibu wa Rais Donald Trump ulitakiwa kusainiwa mjini Washington, Marekani siku ya Ijumaa wiki iliyopita lakini Kongo ilikataa kuusaini katika dakika za lala salama.
Nchi zote zingenufaika na ushirikiano katika sekta ya madini
Mkataba huo ulihimiza miongoni mwa mambo mengine baadhi ya madini kutoka mashariki mwa Kongo yangepelekwa Rwanda na kusafishwa/Kuchakatwa katika viwanda vya Rwanda kabla ya kusafirishwa hadi masoko ya ulaya na Marekani.
Mchakato kuhusu azma hii uliendelea hadi siku ya Ijumaa wiki iliyopita ambapo wajumbe wa Rwanda na Congo walikutana mjini Washington kwa ajili ya shughuli hiyo. Hata hivyo kulingana na serikali ya Rwanda katika dakika za mwisho wajumbe wa Kongo walitakaa kutia saini mkataba huo
Msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo ametoa kauli ndefu kupitia ukurasa wake wa X kwamba wameshangazwa na uamuzi huo wa Kongo. "Tumeshindwa kufahamu sababu hasa ya Kongo kushindwa kusaini mkataba huu katika dakika za mwisho hasa ikizingatiwa jinsi mazungumzo yalivyokwenda katika hali ya uelewano na mshikamano." Amesema Rwanda bado inaamini kwamba kupitia upatanishi wa Marekani mkataba huu utasainiwa.
Rwanda yamshutumu Tshisekedi
Kwa upande wake waziri wa Mambo ya Nje Olivier Nduhungirehe aliyekuwepo mjini Washington siku ya Ijumaa amemlaumu moja kwa moja Rais wa Kongo Felix Tshisekedi.
"Ukweli ni kwamba wajumbe wa Rwanda na DRC kwa wiki nzima walifanya kazi nzuri na kufikia makubaliano mazuri chini ya upatanishi wa Marekani lakini asubuhi iliyofuata yaani siku ya kutia saini, Rais Tshisekedi aliwaamuru watu wake kutosaini mkataba huo," alisema Nduhungirehe.
Lakini wachambuzi wa masuala ya siasa za Maziwa Makuu wanasema hasara ni kwa nchi zote mbili kama ambavyo amesema Emmanuel Kwizera, mwandishi mkongwe na mchambuzi aliyeko huko mjini Kigali. "Wote wangefaidika, kuna faida kwa upande wa Rwanda na kuna faida upande wa Kongo….."
Taarifa zimesema Kongo imeamua kutosaini kama shinikizo kwa Rwanda ikitaka iondoe jeshi lake mashariki mwa Kongo ingawa Rwanda imeendelea kukanusha kuwa na kikosi hicho hali inayowafanya wengi kuamini kuwa huenda mikataba na mazungumzo baina ya pande hizi mbili isizae matunda licha ya shinikizo la Marekani.