Serikali na waasi wakubaliana Jamhuri ya Afrika ya Kati | Matukio ya Afrika | DW | 20.06.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Serikali na waasi wakubaliana Jamhuri ya Afrika ya Kati

Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na makundi 13 kati ya 14 yaliyojihami nchini humo Jumatatu yalisaini makubaliano yanayolenga kufikisha kikomo mapigano ya kikabila na kidini yaliyopelekea vifo vya maelfu ya watu.

Zentralafrikanische Republik Charles Armel Doubane und Armel Mingatoloum Sayo (picture-alliance/AP Photo/D. Stinellis)

Waziri wa mambo ya nje Charles Armel, kulia, akimsalimia mwenzake Armel Sayo baada ya kutia saini makubaliano huko Italia

Makubaliano hayo yaliyosimamiwa na kundi la amani la Saint Egidio kutoka Kanisa Katoliki katika makao yake makuu mjini Roma, yanataka mapigano yasitishwe mara moja na pia yanatoa wito wa kutambuliwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais uliopita.

Makubaliano hayo yaliyojadiliwa katika kipindi cha siku tano, yamesifiwa na kutajwa kama fursa ya kuiimarisha mojawapo ya nchi maskini na zenye machafuko zaidi duniani. Chini ya makubaliano hayo, makundi yaliyojihami yatawakilishwa katika uwanja wa kisiasa na badala yake mashambulizi yasitishwe na wanachama wake watajumuishwa katika jeshi la nchi hiyo.

Jamhuri ya Afrika ya Kati imekumbwa na mapigano ya kidini na kikabila tangu mwaka 2013, pale waasi wa Seleka ambao wengi  ni Waislamu walipochukua mamlaka, jambo lililowafanya waasi wa anti-Balaka ambao wengi ni Wakristo kuanza mapigano.

Makubaliano hayo yatashuhudia kufunguliwa njia zote za mawasiliano

Kundi la Sant Egidio ambalo lilikuwa mpatanishi katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Msumbiji mwaka 1992, limekuwa likijaribu kutafuta amani katika Jamhuri hiyo ya Afrika ya Kati kwa miezi kadhaa. Marco Impagliazzo ni rais wa kundi hilo.

Zentralafrikanische Republik Schulen (picture-alliance/AP Photo/J. Delay)

Mpiganaji wa waasi wa Seleka akirudi kambini

"Leo tumetia saini makubaliano yaliyo na changamoto kubwa kwa pande zote, pamoja na serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na uongozi wake," alisema Marco, "ili kusitishwa kwa mapigano kuafikiwe, na kufunguliwe pia njia zote za mawasiliano ili hatimaye kuwe na uhuru nchini humo."

Makundi ya waasi yaliahidi  kuhakikisha kuna uhuru wa watu kutembea na bidhaa kusambazwa, kwa kuondoa vizuzi kama hatua ya kwanza inayotokana na makubaliano hayo. Pande zote pia zilikubaliana kurejesha mamlaka kwa uongozi wa taifa kote nchini humo. Charles Armel Doubane ni waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliyehudhuria kutiwa saini kwa makubaliano hayo.

Kuna wengine hawaamini iwapo makubaliano hayo yataheshimiwa

"Kwetu sisi haya yamekuwa makubaliano muhimu kwa uwiano nchini mwetu na kwa amani ya baadae katika Jamhuri ya Afrika ya Kati," alisema Armel. "Kwasababu hiyo niko hapa kuiambia jamii ya Sant Egidio, serikali ya Italia na jamii ya kimataifa kwamba, tuliweka juhudi kuhakikisha tunaitimiza ndoto yetu ya pamoja, ambayo ni ndoto ya kuwa na nchi yenye amani."

Zentralafrikanische Republik (DW/A. Kriesch)

Kamanda wa waasi wa anti-Balaka Goumou Passy

Lakini wengine wana ati ati kuhusiana na makubaliano hayo. Philipe Barga mwenye umri wa miaka 40 mjini Bangui, alisema viongozi wa waasi hawakushikilia mikataba waliyotia saini hapo awali. Nikiyanukuu maneno yake,amesema  "ni wale wanaotia saini mikataba hiyo wasiyoiheshimu, siyaamini makubaliano haya," mwisho wa kunukuu.

Mizozo ya kisiasa imeikumba nchi hiyo mara kwa mara na mapigano ya kulipiza kisasi yanaongezeka kwa mara nyengine licha ya uchaguzi wa mwaka jana uliolenga kumaliza umwagikaji damu.

Katika kipindi cha wiki mbili mwezi Mei, mapigano kati ya makundi ya waasi yalipelekea vifo vya watu 300 na kuwaacha wengine 100,000 bila makaazi.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com