Serikali mpya Iraq yapongezwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.09.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Serikali mpya Iraq yapongezwa

Jamii ya kimataifa imekaribisha hatua ya bunge la Iraq kuiidhinisha serikali ya waziri mkuu Haider al-Abadi na kuelezea matumaini kuwa itasaidia juhudi za kupambana na kundi la Dola ya Kiislamu.

Waziri mkuu Abadi alikuwa chini ya shinikizo kuunda serikali shirikishi itakayoweza kushughulikia manun'guniko ya jamii za Wasunni na Wakurdi, ambao walitelekezwa na serikali iliyopita ya waziri mkuu Nouri al-Maliki, na kutoa nafasi kwa kundi la Dola ya Kiislamu kutumia vyema kutoridhika kwao kuteka maeneo makubwa hasa ya Wasunni.

Aapa kufa na IS

Akizungumza mbele ya bunge, waziri mkuu Al-Abadi aliapa kupambana na wapiganaji wenye msimamo mkali wanaodhibiti maeneo makubwa kaskazini na magharibi mwa Iraq. Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry aliwambia waandishi wa habari mjini Washington kuwa Marekani ilipokea vyema habari za kuidhinishwa kwa serikali mpya ya Iraq, na kusema kuwa ina uwezo wa kuziunganisha jamii tofauti za Iraq.

Waziri wa Mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry.

Waziri wa Mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry.

"Likiwa limeweza kuvuka kikwazo cha migawiko ya kikabila na kimadhehebu, bunge la Iraq limeiidhinisha serikali mpya shirikishi, ambayo ina uwezo wa kuwaunganisha Wairaq wote, kwa ajili ya Iraq moja na imara, na kuzipa jamii zake nafasi ya kujenga mustakabali ambao Wairaq wote wanautaka na kustahili," alisema waziri Kerry

Mataifa 40 yaonyesha nia

Waziri Kerry pia alirejea dhamira ya Marekani kuisaidia Iraq kuzitafutia ufumbuzi changamoto zake za kisiasa na kiuchumi, na kukabiliana na kundi la Dola ya Kiislamu. Marekani imekuwa ikifanya mashambulizi ya angani nchini Iraq tangu Agosti 8 na waziri Kerry aliapa kuunda muungano imara wa kimataifa utakaoishinda Dola ya Kiislamu.

Kabla ya kuanza safari yake ya kwenda nchini Saudi Arabia kukutana na mawaziri wa mambo ya kigeni wa matiafa ya Kiarabu, Kerry alisema zaidi ya mataifa 40 yalikuwa tayari kujiunga na muungano huo utakaoongozw ana Marekani

Naye rais wa Iran Hassan Rouhani alieleza matumaini kuwa serikali ya waziri mkuu Haider Al-Abadi itasaidia kulishinda kundi la Dola ya Kiislamu. Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Hossein Amir-Abdollahian alirejea matamshi ya Rouhani, akisema Tehran inaiunga mkono serikali ya Abadi. Licha ya Marekani na Iran kuwa na maslahi sawa ya kulishinda kundi la Dola ya Kiislamu, walikanusha wiki iliyopita kutakuwepo na ushirikiano.

Makamu wa rais wa Iraq Nouri Al-Maliki akimpongeza waziri mkuu Haider Al-Abadi.

Makamu wa rais wa Iraq Nouri Al-Maliki akimpongeza waziri mkuu Haider Al-Abadi.

Nafasi za ulinzi na mambo ya ndani

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon pia alikaribisha hatua hiyo iliyofikia nchini Iraq, lakini aliwataka wanasiasa kujaza haraka nafasi za mawaziri wa ulinzi na mambo ya ndani. Wabunge 289 kati ya 328 walijitokeza na kusaidia kuwaidhinisha manaibu watatu wa waziri mkuu na mawaziri 21.

Abadi aliomba kupewa muda wa wiki moja kuweza kujaza nafasi za mawaziri wa ulinzi na mambo ya ndani, na atakaimu uongozi wa wizara hizo hadi wahusika watakapoteuliwa. Serikali iliyopita pia ilianza huku nafasi nyeti zikiwa wazi na kaimu mawaziri waliishia kuzijaza kwa miaka minne.

Katika hatua ya kuweka urari unaohitajika kuondoa migawiko ya kikabila na kiitikadi iliyokita mizizi nchini Iraq, mahasimu watatu wakubwa waliidhinishwa kama makamu wapya wa rais - mawaziri wakuu wa zamani Nouri al-Maliki na Iyad Allawi, na spika wa zamani wa bunge Osama al-Nujaifi.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe.
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com