Obama kutangaza mpango wa kupambana na IS | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.09.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Obama kutangaza mpango wa kupambana na IS

Rais wa Marekani Barack Obama ametangaza kuwa atazindua mkakati wa kupambana na kulishinda kundi lenye itikadi kali za Kiislamu linalojiita Dola la Kiislamu.

Obama ameyasema hayo wakati Marakeni ikiyaimarisha mashambulizi yake ya angani dhidi ya wanamgambo hao, nayo mataifa ya Kiarabu yakiapa kuchukua “hatua zote muhimu” kukikabili kitisho kinachosababishwa na kundi hilo.

Akizungumza na televisheni ya Marekani ya NBC mwishoni mwa wiki, Rais wa MAREKANI Barack Obama alisema atatoa hotuba Jumatano wiki hii, ili kuzindua “mpango” wa kukabiliana na wanamgambo hao. Amesema "Katika miezi ijayo, tutaweza siyo tu kuzuia kasi ya ISIL, bali pia kuuharibu uwezo wake. Tutayakomboa maeneo linaloyadhibiti na tutalishinda".

Irak Kampf gegen IS

Majeshi ya Iraq yanasaidiwa na mashambulizi ya kutokea angani ya Marekani kupambana na Dola la Kiislamu

Alisema hatatangaza kurejea kwa majeshi ya ardhini ya Marekani nchini Iraq, na badala yake ataangazia zaidi “kampeni ya kupambana na ugaidi”. "Nitaliomba bunge kuhakikisha kuwa linafahamu na kuunga mkono mpango nitakaoutangaza. Na utahitaji raslimali nyingi, nadhani, kuliko kile tunachofanya kwa sasa katika kanda hiyo" Ameongeza rais Obama.

Wakati huo huo, Katibu mkuu wa Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu Nabil al-Arabi, amesema nchi 22 wanachama zimekubaliana kulikabili kundi la IS. Akizungumza na wanahabari mjini Cairo amesema mawaziri wa mambo ya kigeni wa jumuiya hiyo wamekubaliana kuchukua hatua muhimu za kupambana na kitisho hicho.

Marekani yafanya mashambulzii ya kutokea angani

Ndege za kivita za Marekani zimefanya mashambulizi jana katika eneo ambalo wanamgambo wamekuwa wakijaribu kulikamta kutoka kwa majeshi ya serikali na washirika wao wa Kisunni. Taarifa ya jeshi la Marekani imesema makombora hayo yaliyaharibu magari ya kivita, pamoja na maeneo mawili ya kufanyia mashambulizi.

Majeshi ya Iraq yakisaidiwa na makundi ya wapiganaji yaliikomboa wilaya ya Barwana, mashariki mwa Haditha, kutoka mikononi mwa majihadi waliokimbia na kuacha silaha zao na magari.

Jesiden in Sinjar Nordirak 13.08.2014

Wapiganaji wa IS wanatuhumiwa kufanya maovu katika maeneo ya Iraq na Syria ikiwa ni pamoja na mauaji

Mashambulizi pekee ya awali ya Marekani dhidi ya IS nje ya kaskazini mwa Iraq yalifanywa kwa kuiunga mkono operesheni ya jeshi, wapiganaji wa Kishia na wa Kikurdi ili kuwaokoa watu wa jamii ya Yazidi waliyokuwa wamekwama katika mji wa Amerli, kaskazini mwa Baghdad. Serikali za magharibi zinakabiliwa na shinikizo la kuzitaka zichukue hatua kali dhidi ya IS, ambao wanadhibiti maeneo kadhaa ya nchi jirani ya Syria na pia mipaka ya kaskazini na magharibi mwa Iraq.

Katika hatua nyingine muhimu ya mapambano dhidi ya kundi hilo, bunge la Iraq lenye mgawanyiko mkubwa litapiga kura leo kuichagua serikali mpya. Waziri mkuu mteule Haidar al-Abadi anatarajia kuleta utulivu katika siasa zilizogawika za Iraq.

Kumekuwa na miito ya mara kwa mara kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Marekani, ya kuundwa serikali pana yenye kuwajumuisha viongozi wa tabaka zote za jamii ili kupambana na kitisho cha IS.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi Sessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com