IS Watuhumiwa kuangamiza jamii za wachache Iraq | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.09.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

IS Watuhumiwa kuangamiza jamii za wachache Iraq

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limewatuhumu wapiganaji wa kundi la dola la Kiislamu kufanya mauaji ya kikabila kaskazini mwa nchi hiyo ya Iraq.

Wairaqi waandamana bungeni

Wairaqi waandamana bungeni

Shirika la Amnesty International limesema kundi la Dola la Kiislamu limekuwa likiendesha kampeini ya takasatakasa ya kikabila kuwamaliza kabisa watu wa jamii za wachache kaskazini mwa Iraq ikiwemo kuwaua, kuwateka nyara na kutenda uhalifu mwingine wa kivita. Donatella Rovera ni mshauri mkuu kuhusu masuala ya mizozo katika shirika hilo anasema,

''Kundi la Dola la Kiislamu limekuwa likifanya mauaji ya kikabila kwa kiwango kikubwa sana. Wamekuwa wakiwalenga hatua kwa hatua watu wa makabila na dini za walio wachache. Jamii ambazo zimekuwa zikiishi kaskazini mwa Iraq tokea karne kadhaa, wengine wakiwa wameishi huko tangu maelfu ya miaka wamelazimishwa kuyahama makaazi yao, miji yao na hata vijiji vyao.''

Katika ripoti mpya shirika hilo linasema wanamgambo wamewateka nyara mamia ikiwa sio maelfu ya wanawake na watoto kutoka jamii ya Wayazidi. Pia wanamgambo hao wa itikadi kali wanatajwa kuwazingira wanaume wa jamii hiyo ya Wayazidi pamoja na vijana kabla ya kuwaua. Ripoti hiyo iliyotolewa leo inatowa ushahidi zaidi kuhusu uhalifu mkubwa unaofanywa na kundi hilo tangu lilipoanza kutanua hujuma zake kutokea Syria hadi kwenye eneo zima la nchi jirani ya Iraq mnamo mwezi Juni. Wanamgambo hao wameliteka eneo kubwa la kaskazini na magharibi mwa Iraq na limeweza kujitanua hadi kufikia viungani mwa mji mkuu wa Iraq Baghdad. Shirika la Amnesty International kwa hivyo linazungumzia wasiwasi wa hali iliyopo na hatma ya jamii za wachache katika Iraq.

''Lakini hatufahamu nini kitatokea baadaye, ikiwa kundi hili litafanikiwa kuyadhibiti maeneo mengine. Kuna kila sababu ya kuamini kwamba watachukua hatua kama waliochukua huko nyuma, kwa sababu hicho ndicho kitu wanachokifanya hatua kwa hatua katika kila mji.''

Vikosi vya Peshmerga Kaskazini ya Iraq

Vikosi vya Peshmerga Kaskazini ya Iraq

Jumatatu baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha ombi la Iraq la kuanzisha uchunguzi juu ya madai hayo ya uhalifu wa kivita unaodaiwa kufanywa na kundi la dola la Kiislamu dhidi ya raia. Hatua hiyo inakusudiwa kutoa ripoti kamili kwa baraza hilo la haki za binadamu pamoja na ushahidi unaoweza kutowa mwangaza zaidi juu ya mauaji ya wairaqi na kutumiwa kama sehemu ya ushahidi katika kesi yoyote ya uhalifu itakayofunguliwa kwenye korti ya Kimataifa.

Katika ripoti yake shirika la Amnesty International inaeleza kwa undani jinsi wapiganaji wa dola la kiislamu walivyowafukuza wakristo, washia, wayazidi na jamii nyinginezo kutoka majumbani mwao.

Wakati huo huo, taarifa kutoka ndani ya Iraq zinasema vikosi vya usalama vya Iraq vimefanikiwa kutwaa udhibiti wa sehemu ya barabara kuu inayounganisha mji wa Baghdad na Kaskazini mwa Iraq. Halikadhalika miji mingine miwili ya kaskazini mwa Amerli ilikombolewa kutoka mikononi mwa wapiganaji hao wa jihad kwa usaidizi wa mashambulio yaliyofanywa na ndege za Marekani.

Ushindi huo wa vikosi vya Iraq ndio wa kwanza tangu jeshi hilo lilipozidiwa nguvu katika maeneo mengi ya kaskazini mwa Iraq mnamo mwezi Juni ambapo kiasi ya wanajeshi 1700 waliishia kukamatwa na wapiganaji hao huku ikiaminika kwamba wengi wao waliuwawa. Polisi wa kukabiliana na fujo wamejaribu kuwatimua mamia ya waandamanaji waliovamia bunge mjini Baghadad wakitaka baadhi ya maafisa wamebebeshwe dhamana ya kutoweka wanajeshi hao.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/AP/AFP

Mhariri:Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com