Schulz ataka kuinusuru kampeni ya SPD | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.06.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Schulz ataka kuinusuru kampeni ya SPD

Kiongozi wa chama cha Social Demokrat Martin Schulz amemshutumu Kansela Angela Merkel kwa kiburi wakati akiwa katika juhudi za kubadili kushuka kwa umashuhuri wa chama chake kabla ya uchaguzi mkuu.

Uamuzi wa Schulz kushika hatamu za uongozi wa chama chake awali ulikipa uhai mpya chama cha SPD lakini mwenendo huo umerudi nyuma.

Ikiwa zimebakia wiki chache kabla ya Wajerumani kupiga kura hapo Septemba 24 chama cha SPD kiko nyuma ya chama cha Merkel cha Christian Demokrat kwa alama za asilimia 15 kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliochapishwa Jumapili na gazeti la Ujerumani la Bild am Sonntag.

Schulz alikuwa katika hisia ya mapambano katika mkutano huo maalum wa wanachama wa chama chake kuidhinisha programu yao ya kampeni kwa maneno makali dhidi ya Merkel ambaye amemshutumu kwa kukataa moja kwa moja mdahalo juu ya mustakbali wa taifa.

Amesema mbinu ya Merkel ni kuendelea kushikilia kutowa maoni yake badala ya kuwasiliana na wengine na hiyo kuwafanya watu wasiwe na utashi katika siasa.

Kiburi cha madaraka

Deutschland SPD Programmparteitag in Dortmund | Martin Schulz umarmt Gerhard Schröder (picture alliance/dpa/J. Güttler)

Kiongozi wa SD Martin Schulz akiwa na Kansela wa zamani wa Ujerumani Gerhard Schröder wa chama cha SPD.

Schulz amesema wakati chama hicho cha SPD kinakuwa na msimamo katika masuala upande wa pili uko kimya.Shulz ambaye chama chake ni mshirika mdogo wa seikali ya mseto ya Merkel amekiita kitendo hicho kuwa ni shambulio dhidi ya demokrasia  na kuonya "hatari kubwa kabisa ni kiburi cha madaraka."

Schulz amesisitiza shinikizo la chama chake kwa "haki ya kijamii"  kwa kutoza kodi kubwa wenye kipato kikubwa na shule bure kwa wote.

Pia ameliweka suala la ndoa za mashoga kuwa sharti la kuundwa kwa serikali yoyote ya mseto huko mbele ikayokihusisha chama chama cha SPD.

Spika huyo wa zamani wa bunge la Ulaya mwenye umri wa miaka 61 alieshangiliwa kwa dakika kumi kwa hotuba yake ya dakika 90 amesema "Sitosaini makubaliano ya serikali ya mseto ambayo kwayo ndoa za mashoga hazitojumuishwa."

Wito huo wa chama cha SPD kwa ndoa ya mashoga unakuja wiki moja tu baada ya chama cha Kijani kuweka sharti hilo hilo na hiyo kuweka shinikizo kwa chama cha Merkel cha CDU ambacho hadi sasa kimekataa kuruhusu watu wa jinsia moja kuowana.

 

Kufufuwa umashuhuri wa chama

Deutschland SPD Programmparteitag in Dortmund (picture alliance/dpa/J. Güttler)

Wanachama wa SPD katika mkutano wao mkuu maalum huko Dortmund.

Chama cha SPD kinataraji programu yake ya kampeni itakisaidia kurudisha umashuhuri lakini Schulz mwenyewe ameonya kuwa safari ni ngumu huko mbele bada ya chama chake kushindwa vibaya katika chaguzi tatu za majimbo mfululizo.

Kwa wachambuzi kushuka ghafla kwa uungaji mkono wa chama cha SPD cha Schulz kumetokana na mafanikio ya serikali kudhibiti wimbi la wakimbizi ambalo limeshuhudia kuwasili kwa wahamiaji 890,000 nchini hapo mwaka 2015 na kuwaudhi wapiga kura wengi wa Ujerumani.

Gero Neugebauer mchambuzi wa taaluma ya siasa katika Chuo Kikuu Huria cha Berlin amesema Schulz awali aliwasilishwa kama mbadala kwa Bibi.Merkel na alikuwa ni mtu mpya kabisa na alikuwa akishutumu sera ya uhamiaji ya Merkel ambayo iligawa maoni ya watu.

Renate Koechner wa kundi la utafiti wa maoni la Taasisi ya Allensbach ameandika katika gazeti la Frankfurter Allgemeine kwamba lakini suala la kuwasili kwa wahamiaji limepowa na chama cha Merkel na chama ndugu cha CSU vimezidi kuaminiwa na vina mkakati bora kukabiliana na hali ya wakimbizi.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Caro Robi

                                                               

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com