Ruto tayari kuzungumza na Kenyatta bila masharti | Matukio ya Afrika | DW | 17.09.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Ruto tayari kuzungumza na Kenyatta bila masharti

Makamu wa Rais nchini Kenya William Ruto amesema yuko tayari kumaliza msuguano uliojitokeza kati yake na Rais Uhuru Kenyatta bila ya masharti yoyote.

Utengano kati ya rais Kenyatta na makamu wake William Ruto, sio suala la siri, lakini ni taswira ambayo imekuwa ikionekana wazi, wakati rais Kenyatta akisema  hafahamu chanzo chake, Ruto amekuwa akimnyoshea kidole cha lawama kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kuvuruga mahusiano yao na Rais.

Uhasama kati yao, umesababisha, hali ya hofu katika taifa ambalo linakaribia kufanya uchaguzi na lenye historia ya machafuko kila wakati uchaguzi unapoandaliwa. Ruto anakua wa kwanza kuitikia  wito wa maaskofu wa kanisa katoliki wa kufikia maridhiano.

"Mimi niko tayari. Hawa maaskofu wamesema wanataka kuniweka pamoja na rais. Mimi niko tayari asubuhi na mapema bila masharti. Kwa sababu mimi ninamuheshimu rais yeye ni kiongozi wangu.”, alisema Ruto

Upatanishi wa kanisa katoli

Mwezi uliopita Rais Kenyatta alimhimiza Makamu wake kujiuzulu iwapo haridhishwi na utendaji kazi wa serikali. Kiyume chake  Ruto aliapa kwamba hatojiuzulu kwani hatua hiyo ingemwonesha kuwa mwanasiasa  mwoga na msaliti. Lakini Yumkini matamshi ya Maaskofu 23 wa kanisa katoliki waliofanya mkutano chini ya mwavuli wa Kongamano la Maaskofu wa Kanisa Katoliki yamelegeza moyo wa Ruto ambaye mahasimu wake wa siasa wamemtaja kuwa na msimamo dhabiti. Anthony Muheria ni Askofu wa jimbo la Nyeri.

"Huenda kuna mambo mengi hatuyafahamu, tunasema ni ishara mbaya. Hata katika familia mama na baba wanapokwaruzana, watoto wanaangalia na kusema mambo si mazuri.”, alisema Muheria.

Soma pia: ◙Rais Kenyatta amtaka Makamu wake Ruto kujiuzulu

''Sina ufahamu wa kitu chochote''

Ruto amekuwa akikosekana kwenye mikutano muhimu ya serikali. Hivi karibuni rais wa Estonia Kersti Kaljulaid alipofanya mazungumzo ya ushirikiano na rais Kenyatta katika ikulu ya Nairobi, Ruto hakuwepo.

Viongozi wa kanisa katoliki walishinikizwa na matukio kama hayo kujitoa kuongoza juhudi za upatanisho kati ya rais na makamu wake. Ikulu haijatoa tamko kuhusu wito huo, hata hivyo Rais Kenyatta alinukuliwa akisema kuwa Ruto anaikosoa serikali.

"Sina ufahamu wa kilichotokea, pengine anajaribu kujenga msingi wa siasa zake za baadaye, ambayo ni haki yake, sijawahi kumkanya, lakini nadhani njia ambayo anatumia sio sawa.”, alisema Kenyatta.

Uhasama kati ya Rais Kenyatta na Makamu wake Ruto zilizidi wakati kiongozi wa taifa hilo la Kenya, aliposalimiana na hasimu wake wa siasa Raila odinga mwezi Machi mwaka 2018 kwenye tukio maarafu lililofahamika kama handshake, baada ya kuzika tofauti zao baada ya uchaguzi mkuu wenye utata uliofanywa mwaka 2017, ambapo Raila alidai kuwa aliibiwa kura.