1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UfisadiKenya

Ripoti: Polisi Kenya bado yakumbwa na jinamizi la ufisadi

28 Februari 2024

Ripoti ya jopo kazi la masuala ya utendaji wa polisi nchini Kenya imebainisha kuwa idara ya polisi nchini humo inaandamwa na shutuma kali za kuendekeza ufisadi.

https://p.dw.com/p/4cxft
Kenya | Polisi kwenye maandamano Nairobi
Ripoti ya kamati ya Jaji Maraga inaonyesha Polisi nchini Kenya bado inakabiliwa na tatizo kubwa la ufisadi.Picha: YASUYOSHI CHIBA/AFP

Ripoti ya jopo kazi la masuala ya utendaji wa polisi nchini Kenya imebainisha kuwa idara ya polisi nchini humo inaandamwa na shutuma kali za kuendekeza ufisadi hata baada ya serikali kuwekeza katika kuimarisha utendaji wake.

Baadhi ya maovu yaliyotajwa ni kuuza nafasi za ajira, ukabila na upendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari, katibu katika wizara ya usalama wa taifa Raymond Omollo alitangaza kuwa maafisa wa polisi wataongezwa mshahara kwa awamu.

Kamati hiyo ya watu 20 iliwasilisha ripoti kwa Rais William Ruto mwezi Novemba mwaka uliopita. Ripoti hiyo imewanyooshea kidole cha lawama maafisa wa ngazi ya juu wanaotumia njia zisizofaa kuajiri polisi wapya.

Kenya Nairo| Rais wa Kenya William Ruto na Makamu wake Rigathi Gachuaga.
Rais William Ruto, katikati, na makamu wake Rigathi Gachuaga katika mkuwano mjini Nairobi. Ruto aliahidi kupambana na rushwa ndani ya jeshi la polisi.Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Soma pia: Waziri wa fedha Kenya akamatwa

Baadhi wanajigawia nafasi hizo za ajira na kuwapa watakaowatoza hela nyingi kiasi ya shilingi laki sita za Kenya. Kitendo hicho kinaubeza uteuzi unaofanyika hadharani katika kila kaunti pindi wanapozitangaza nafasi hizo.

Hati hiyo imebainisha kuwa kwa muda wa miaka 15 ambayo serikali imewekeza kuimarisha utendaji wa idara ya polisi, hali bado si hali. Waziri wa usalama wa taifa Kithure Kindiki akiwa Mombasa alionya kuwa maafisa wabaya hawatavumiliwa.

Idara ya polisi inashutumiwa kwa kukiuka sheria, kutumia nguvu kupita kiasi na ukatili, kuegemea upande mmoja wakati wa uchaguzi na udhalilishaji kati ya maafisa wa ngazi ya juu na polisi wa madaraja ya chini.

Soma pia: Ripoti kuhusu viwango vya ufisadi duniani yatolewa

Kwa mujibu wa katiba, uteuzi wa maafisa wa polisi unapaswa kuwa na uwazi, ushindani na unaozingatia uwezo pamoja na kutimiza vigezo vya elimu na tajiriba. Badala yake mchakato huo unazongwa na upendeleo, ukabila na ufisadi.

Mgongano wa kimaslahi miongoni mwa vigogo

Kamati hiyo ya Jaji mkuu mstaafu David Maraga imebaini kuwa upo mgongano wa maslahi kwenye idara hiyo ya polisi ukizingatia kuwa baadhi ya maafisa wanaendesha biashara ya huduma za usafiri wa umma na uvutaji wa magari yaliyoharibika, kuuza pombe, vibanda vya kamare na biashara nyengine ambazo zinaathiri utendaji wao na maadili ya kikazi.

Soma pia: Kenya: Polisi wawakimbia maafisa wa kupambana na rushwa

Kwa upande wake Inspekta Mkuu wa Polisi, Japhet Koome ameitaka serikali kuu kuwapa wajibu wa kutoa vibali vya kuuza pombe nchini.

Jopo hilo limependekeza suluhu ambayo ni kuunda kitengo maalum cha polisi wa usalama barabarani kilicho na maafisa maalum wachache walio na ujuzi na teknolojia na pia vituo vya barabarani kuondolewa.

Vita dhidi ya ufisadi michezoni Kenya

Kadhalika faini zilipwe kwa mifumo ya kisasa kupunguza uwezekano wa kujilimbikia pesa taslimu.

Jopo limependekeza pia vituo vya polisi barabarani kuondolewa katika kipindi cha miezi sita na majukumu yake kukabidhiwa kikosi cha magari ya uangalizi. Tathmini hiyo imefanyika kwenye kaunti zote 47.

Soma pia: Wizara ya Usalama Kenya yatajwa kuwa fisadi zaidi, ripoti

Ripoti imependekeza uteuzi wa makamanda kuzingatia tajiriba, uwezo na elimu badala ya wajibu huo kutimizwa na rais. Ili kuwatia moyo maafisa, mapendekezo yamejumuisha pia nyongeza ya mshahara kwa maafisa.