1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wizara ya Usalama Kenya yatajwa kuwa fisadi zaidi, ripoti

Shisia Wasilwa, DW, Nairobi19 Novemba 2019

Wizara ya usalama wa taifa nchini Kenya inaongoza kwenye visa vya ufisadi kutokana na mifumo duni na ukosefu wa maadili. Hayo ni kwa mujibu wa tume ya Kitaifa ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini humo.

https://p.dw.com/p/3TKXn
Kenia | Drogenhandel | Fred Matiang'i
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Wizara ya Usalama wa Kitaifa imetajwa kuwa fisadi zaidi nchini Kenya kwa mujibu wa ripoti ya Tume ya Kitaifa ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini humo. Ripoti hiyo iliyotolewa leo, imesema kuwa nusu ya visa vyote vya ufisadi vinavyoripotiwa nchini humo hutokea katika wizara hiyo.

Wizara ya usalama wa taifa inaongoza kwenye visa vya ufisadi kutokana na mifumo duni na ukosefu wa maadili. Asilimia 47.5 ya wakenya walioulizwa walisema wamewahi kuombwa rushwa walipokuwa wakitaka huduma katika wizara hiyo. Hali hiyo hufanyika kutokana mmoja anayetaka huduma za haraka ama kukwepa mkono mrefu wa sheria.

Idara ya kuwasajili watu ilitajwa na tume hiyo kuwa fisadi zaidi miongoni mwa taasisi hiyo. Katika kikundi cha watu 10, watu saba hutoa hongo ili kupata huduma za serikali. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya watu wanaotoa hongo kwa serikali imeongezeka kutoka asilimia 35 mwaka 2015 na sasa ni asilimia 73.

"Idara inayoonekana kuwa fisadi zaidi serikalini kama kawaida ni idara ya polisi, ambayo haijabadilika asilimia 39.6, inafuatiwa na shirika la Nguvu za umeme.” Amesema Vinicent Okong'o ambaye ni Mkurugenzi wa tume hiyo.

Mwenyekiti wa tume ya Maadili na kupambana na ufisadi Kenya Eliud Wabukhala (Kushoto) na Mkurugenzi mtendaji wa tume hiyo Twalib Mubarak (Kulia)
Mwenyekiti wa tume ya Maadili na kupambana na ufisadi Kenya Eliud Wabukhala (Kushoto) na Mkurugenzi mtendaji wa tume hiyo Twalib Mubarak (Kulia)Picha: picture-alliance/dpa/Photoshot/C. Onyango

Taasisi nyingine za serikali ambazo zilitajwa kwenye ripoti hiyo ya ufisadi ni pamoja na hospitali za umma, serikali za kaunti na wizara ya elimu.

Wizara ya Ardhi na Uchukuzi pia zimetajwa kwenye ripoti hiyo kuwa na visa vya ufisadi. Katika wizara ya kilimo udanganyifu, kuidhinishwa kwa ujenzi haramu wa majengo, kupotea kwa faili na utapeli, ni masuala yaliyotajwa kufanyika katika wizara hiyo. Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi ilifichua kuwa Halmashauri ya Kusimamia Ardhi imeshindwa kutambua wamiliki halali wa ardhi wakati wa ununuzi na uuzaji.

" Tunataka sheria itakayoturuhusu kuangalia utajiri wa fedha wa mtu, ili mtu akitangaza mali yake, mashirika yote ya kukabiliana na ufisadi yanaweza kujua.” Amesema Eliud Wabukala ambaye ni mwenyekiti wa Tume hiyo.

Uchunguzi huo kuhusu ufisadi wa mwaka 2018, ulifanywa na tume ya Kitaifa ya Maadili na Kupambana na ufisadi- EACC
Uchunguzi huo kuhusu ufisadi wa mwaka 2018, ulifanywa na tume ya Kitaifa ya Maadili na Kupambana na ufisadi- EACC

Tume hiyo imependekeza matumizi ya dijitali kwenye wizara ya ardhi ili kukabiliana na usimamizi duni wa nyaraka za ardhi. Ripoti hiyo imetaja kuwa wizara ya ardhi haina mipango mizuri ya kuidhinisha utekelezaji wake.

Ufisadi ni jinamizi baya ambalo linapatikana katika nusu ya matatizo yanayowazonga wakenya huku viwango vya ukosefu wa ajira vikiongezeka, gharama ya maisha ikipanda na uchumi ukiendelea kudorora.

Utafiti wa ripoti ya ufisadi ya mwaka 2018, ulifanywa kati ya tarehe 16 mwezi Novemba na tarehe 19 mwezi Desemba mwaka huo. Utawala wake rais Kenyatta umekumbwa na visa vingi vya ufisadi zaidi ya watangulizi wake.