1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Jemen Feuerpause, Rede Abedrabbo Mansour Hadi
Picha: YEMEN TV/AFP via Getty Images

Rais wa Yemen akabidhi madaraka kwa baraza jipya la uongozi

Zainab Aziz Mhariri: Chilumba Rashid
7 Aprili 2022

Rais Abedrabbo Mansour Hadi amekabidhi madaraka yake kwa baraza jipya la uongozi katika hatua kubwa ya mabadiliko kwenye muungano unaopambana na waasi wa Houthi.

https://p.dw.com/p/49bWG

Rais wa wa Yemen Abedrabbo Mansour Hadi amesema hayo katika televisheni siku ya Alhamisi, ikiwa ni siku ya mwisho ya mazungumzo ya amani yaliyokuwa yanafanyika katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh. Rais Hadi pia amemwondoa madarakani makamu wake wa rais Ali Mohsen al-Ahmar.

Mjumbe Maalum wa Marekani kwa Yemen Tim Lenderking akihutubia kwenye mkutano kuhusu vita vya Yemen katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh.
Mjumbe Maalum wa Marekani kwa Yemen Tim Lenderking akihutubia kwenye mkutano kuhusu vita vya Yemen katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh.Picha: Fayez Nureldine/AFP

Mansour Hadi amesema amechukua hatua hiyo ili kuwashirikisha viongozi madhubuti katika kuisimamia serikali kwenye awamu hii ya mpito, na pia kuthibitisha dhamira ya serikali yake ya umoja, mamlaka, uhuru, na uadilifu kwa taifa la Yemen na kulinda usalama wa Yemen.

Baraza jipya litakaloongozwa na Meja Jenerali Dk. Rashad al-Alimi, litasimamia kwa muda sekta ya siasa, kijeshi na usalama wa Yemen katika kipindi cha mpito.

Mkuu wa baraza jipya la uongozi atapewa usaidizi na wajumbe wengine saba: Wajumbe hawa watashikilia cheo cha Naibu Mwenyekiti wa Uongozi wa Rais utakaoshirikiana na tume ya wajumbe 50 ambao watatoa ushauri kwa serikali hiyo ya mpito sambamba na kamati nyingine ya wajumbe wanane.

Jemen Deutschland Sanaa Sicherheitsminister Rashad al-Alimi zu Geiseln
Picha: picture alliance / dpa

Pia kuna makundi tofauti ya kisheria na kiuchumi. Baraza hilo la mpito litamaliza muda wake baada ya kuchaguliwa rais mpya. Kulingana na agizo la rais, baraza hilo jipya lina mamlaka ya kufanya mazungumzo na wawakilishi wa Houthi ili kupata suluhu ya mgogoro wa nchini Yemen.

Kwa mujibu wa amri ya Rais, baraza hilo la mpito limepewa mamlaka ya kupitisha sera ya kigeni, kuimarisha usalama wa taifa, kufanya mabadiliko ya kupambana na ugaidi, kuanzisha mahusiano ya kidiplomasia, kuweka hali ya hatari inapohitajika, kuwateua magavana, wakurugenzi wa usalama, na majaji wa mahakama kuu.

Wapiganaji wanawake wa Yemen wanaowaunga mkono waasi wa Houthi.
Wapiganaji wanawake wa Yemen wanaowaunga mkono waasi wa Houthi.Picha: Mohammed Huwais/AFP

Rais wa Yemen anayeondoka Abedrabbo Mansour Hadi anauachia wadhifa huo miaka 10 tangu alipochaguliwa mnamo mwaka wa 2012. Serikali yake iliyotambuliwa kimataifa imekuwa katika mzozo na waasi wa Kihuothi wanaoungwa mkono na Iran ambao wanaudhibiti mji mkuu wa Yemen, Sanaa Pamoja na sehemu kubwa ya kaskazini licha ya mapambano ya majeshi ya muungano yanayoongozwa na Saudi Arabia yalioanzishwa mnamo mwaka 2015.

Chanzo:AFP