1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaVisiwa vya Comoros

Rais wa Comoro Azali Assoumani aapishwa kwa muhula wa nne

26 Mei 2024

Rais Assoumani ameahidi kufanya kila awezalo kwa ajili ya amani na kukuza uchumi wa visiwa hivyo baada ya kuapishwa kuhudumu kwa muhula wake wa nne madarakani.

https://p.dw.com/p/4gIU8
Rais wa visiwa vya Comoro Azali Assoumani katika mkutano kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya mjini New Delhi
Rais wa visiwa vya Comoro Azali Assoumani katika mkutano kati ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya mjini New DelhiPicha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Rais wa visiwa vya Comoro Azali Assoumani ameahidi kufanya kila awezalo kwa ajili ya amani na kukuza uchumi wa visiwa hivyo baada ya kuapishwa kuhudumu kwa muhula wake wa nne madarakani kufuatia uchaguzi wa Januari uliogubikwa na madai ya wizi wa kura.

Katika hafla ya kuapishwa kwake iliofanyika katika uwanja wa michezo mji mkuu wa Moroni, Rais Assoumani amewashukuru raia wa kisiwa hicho kwa kuonyesha imani naye na kuuhimiza upinzani na wanasiasa kuweka kando tofauti zao kwa ajili ya amani na demokrasia.

Soma pia: Comoro yakataa kuwapokea wahamiaji wa Mayotte

Katika hotuba yake, kiongozi huyo ambaye aliwahi pia kuwa mwanajeshi, amesema mizozo baada ya uchaguzi hutokea kila sehemu na wala sio visiwani humo tu. Ameongeza kuwa ataweka mikakati ya kukuza uchumi wa visiwa hivyo kwa asilimia 5 kila mwaka.

Mtu mmoja alikufa na wengine 25 walijeruhiwa katika maandamano ya vurugu yaliyozuka Comoros baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza Azali Assoumani kama mshindi wa uchaguzi kwa kupata asilimia 63 ya kura.