Rais Park Geun-Hye aahidi ya enzi mpya Korea Kusini | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.12.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rais Park Geun-Hye aahidi ya enzi mpya Korea Kusini

Rais mpya wa Korea Kusini Park Geun-Hye, ambaye ni mwanamke wa kwanza kuiongoza nchi hiyo, ameahidi kusimama imara kuhusu suala la usalama wa taifa hilo, licha ya kutaka kushirikiana kwa karibu zaidi na Korea Kaskazini.

Rais mpya wa Korea Kusini Park Geun-hye.

Rais mpya wa Korea Kusini Park Geun-hye.

Katika hotuba ya kwanza ambamo amebainisha vipaumbele vya sera yake baada ya kutangazwa mshindi hapo jana, Park amesisitiza kitisho kikubwa kinachotolewa na Korea kaskazini kwa usalama ambacho kilidhihirishwa na hatua ya nchi hiyo kuzindua roketi ya angani wiki iliyopita. Aliahidi pia kufanya kazi kuhakikisha utulivu wa eneo la kaskazini mashariki mwa Asia, ambako Korea Kusini, China na Japan zinazozania maeneo.

Rais mpya wa Korea Kusini Park Geun-Hye.

Rais mpya wa Korea Kusini Park Geun-Hye.

Park aliwaambia wakorea kuwa atasimamia ahadi yake ya kuanzisha enzi mpya katika rasi ya Korea, katika misingi ya usalama imara na diplomasia ya kuaminiana. Wakati wa kampeni yake, Park alijitenga na msimamo mkali wa rais anaemaliza muda wake Lee Myung Bak, ambaye alisimamisha misaada muhimu ya kibinadamu kwa ndugu zao wa kaskazini. Park aliahidi sera ya ushirikiano na Korea na Kaskazini, na hakuondoa uwezekano wa kufanya mkutano na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, aliyeingia madarakani mwaka mmoja uliyopita.

Vikwazo vinavyomkalbili

Wachambuzi wanasema atazuiwa na watu wenye msimamo mkali ndani ya chama chake cha kihafidhina cha New Frontier, na pia jumuiya ya kimataifa inayolenga kuiadhibu Korea Kaskazini kwa kile ilichokiona kama jaribio la kombora la masafa marefu kwa kisingizio cha kutuma roketi angani. Afisa kutoka taasisi ya ushauri ya Sejong, Hong Hyuk-Ik amesema kutoka na msimamo juu ya utawala mjini Pyongyang na uzinduzi wa roketi hivi karibuni, Park hatakuwa wa kwanza kuchukua hatua ya kuboresha uhusiano na kaskazini. Lakini ameongeza kuwa rais huyo hatapinga kama utawala wa rais Obama utachukua hatua ya kuishirikisha Korea kaskazini katika majadiliano baada ya kutulia kwa kelele dhidi ya uzinduzi wa roketi.

China, ambayo ndiyo mshirika muhimu na mkubwa pekee wa Korea Kaskazini, na tegemeo la kiuchumi kwa taifa hilo, ilimpongeza Park kwa kuchaguliwa kwake na kushinikiza maboresho katika uhusiano kati ya Seoul na Pyongyang. Park aliahidi kujenga hali ya kuaminiana katika eneo la kaskazini mashariki mwa Asia, lakini katika hatua iliyoilenga zaidi Japan, alisisitiza kuwa utulivu laazima uzingatie utambuzi sahihi wa kihistoria.

Aliyekuwa mpinzani wa Park, Moon Jae-In.

Aliyekuwa mpinzani wa Park, Moon Jae-In.

Mizozo ya maeneo kaskazini mashariki mwa Asia

Korea Kusini na Japan ziko katika mgogoro juu ya kundi la visiwa vidogo vinavyodhibitiwa na Korea Kusini vilivyoko katika bahari ya Japan. Japan pia ina mgogoro tofauti lakini unaofanana na huo na China. Kuna wasiwasi nchini Korea Kusini, ambako bado kuna kumbukumbu mbaya ya kutawaliwa na Japan kuanzia mwaka 1910 hadi 1945, juu ya kuongezeka kwa uzalendo nchini Japan chini ya waziri mkuu mpya Shinzo Abe.

Ushindi wa Park dhidi ya mpinzani wake, mliberali Moon Jae-In kwa asilimia 51.6 dhidi ya 48.0 kunaonyesha jinsi wapiga kura nchini humo walivyogawanyika. Park ni mtoto wa mtawala wa zamani wa kijeshi nchini Korea Kaskazini Park Chung-Hee, ambayo aliitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma kati ya mwaka 1961-1979.

Utawala wake ulikuwa na shabaha mbili --- kuilinda nchi dhidi ya Korea Kaskazini na maendelea ya kiuchumi. Alifanikiwa kwa yote, lakini kupitia ukandamizaji wa wapinzani. Urithi huu wa Park ulizozonga kwa kiasi kikubwa kampeni za binti yake, na katika jitihada za kuleta maridhiano, alitambua hadharani ukiukaji chini ya utawala wa baba yake na kuziomba radhi familia zilizoathirika.

Rais wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un.

Rais wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un.

Aahidi kuunganisha raia wa nchi hiyo

Siku ya Alhamis asubuhi,Park alizuru kaburi la baba yake na pia la moja wa wakosaoji wakubwa wa baba yake na mpinzani wake wa kisiasa, rais wa zamani Kim Dea-Jung, na kuahidi kuodoa mgawanyiko uliyolikumba taifa hilo katika nusu karne iliyopita.

Wakati Korea Kaskazini na mizozo mingine ya kanda itakuwa vipaumbele vya sera yake ya kigeni, changamoto ya kwanza ya Park ni masuala ya ndani ambayo yaligubika kapeni za uchaguzi. Wakati ambapo mdororo wa uchumi wa dunia unazidi kuathiri biashara ya nje, kasi ya ukuaji wa uchumi wa Korea Kaskazini imekuwa ya kusuasua, na pengo kati ya maskini na matajiri linazidi kuongezeka.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Saum Yusuf

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com