Rais Kagame apewa nafasi kubwa kushinda uchaguzi Rwanda | Matukio ya Afrika | DW | 24.07.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Rais Kagame apewa nafasi kubwa kushinda uchaguzi Rwanda

Rwanda ikiwa katika hatua za mwisho kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa August 4 mwaka huu, basi ni dhahiri kuwa Rais wa nchi hiyo Paul Kagame atashinda uchaguzi huo.

Hali  inaonesha kuwa upinzani hauna nafasi ya kushinda uchaguzi huo huku pia vyombo vya habari vya nchi hiyo ambavyo vingi vinadhibitiwa na serikali vikionesha kuegemea zaidi kwa Rais Paul Kagame pamoja na chama chake cha RFP.

Wagombea  wengine wawili wameruhusiwa kuwania urais katika kinyan'ganyiro hicho ambao ni Frank Habineza, mwenyekiti wa chama cha Green Party  na mgombea mwengine anayewania kama mgombea anayejitegemea na ambaye pia anafahamika kwa kiwango kidogo Philippe Mpayimana ambaye ni mwandishi wa habari wa zamani aliyerejea hivi karibuni nchini Rwanda baada ya kuishi miaka kadhaa uhamishoni katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na nchini Ufaransa.

Wagombea wengine waliojitokeza wakiomba kupitishwa kuwania nafasi hiyo waligonga mwamba baada ya kushindwa kutimiza masharti kadhaa ikiwa ni pamoja na kushindwa kufikisha idadi inayohitajika ya sahini za kudhaminiwa. Mgombea mwengine alilazimika kujiengua baada ya picha zake za siri kuchapishwa mtandaoni.

Kagame alilazimika kubadilisha katiba

Ili Rais Kagame aweze kuwania muhula wa tatu wa uongozi alilazimika kufanya mageuzi kadhaa kwani  katiba ya Rwanda awali haikuruhusu Rais kuhudumu muhula wa tatu madarakani. Mwezi Oktoba 2015 bunge la nchi hiyo liliridhia marekebisho ya katiba  yaliyompa nafasi Kagame kuwania tena nafasi hiyo katika uchaguzi wa mwaka 2017, 2024 na 2029. Kinadharia inaonesha kuwa atasalia madarakani kama Rais hadi mwaka 2034.

Bunge la Seneti nchini humo lilipiga kura kuridhia mabadiliko hayo ya katiba ambayo pia yaliungwa mkono na umma katika kura ya maoni.

" Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo Rwanda ni nchi ya kidemokrasia  lakini imekuwa ikiongozwa na utawala wa kiimla chini ya Rais Paul Kagame  na ni nchi yenye viashiria vya utawala wa kiditeta" anasema Hankel mchambuzi wa siasa za Rwanda.

Rais Kagame awali alitangaza hapo kabla kuwa atastaafu baada ya kumalizika  muhula wake wa tatu mwaka 2024.  Hata  hivyo Henkel  bado anaamini kwamba bado Kagame anaweza akaingia majaribuni akaendelea kubakia madarakani

Warteschlangen bei den Wahlen in Ruanda (picture-alliance/dpa)

Baadhi ya wapiga kura nchini Rwanda wakijiandaa kupiga kura uchaguzi uliopita

.

Awali Kagame alisema  atawania nafasi hiyo kwa vipindi viwili tu vya miaka 14 lakini hata hivyo hakutimiza ahadi yake hiyo na kuna hatari kubwa iwapo hataondoka madarakani. Hata hivyo licha ya kukumbana na ukosoaji kuhusiana na hali ya kibinadamu nchini humo bado Rais Kagame anasifiwa kwa mafanikio  kiuchumi.

Mwandishi: Isaac Gamba/dw

Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com