Qatar iko tayari kwa mazungumzo | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.07.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Qatar iko tayari kwa mazungumzo

Mfalme wa Qatarametoa wito wa majadiliano ijumaa(21.07.2017)kutatua mzozo wa kisiasa baina ya nchi yake na mataifa ya kiarabu, akisema mazungumzo yanapaswa kuheshimu mipaka ya nchi,wito huo hauonekani kumaliza mzozo huo.

Katika  hotuba yake ya kwanza  tangu mataifa manne  ya  Kiarabu kuvunja  uhusiano  na  Doha, amesema  Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani katika  hali  ya  kukaidi kwamba  maisha  yanaendelea  kama kawaida  licha  ya  kile  alichokieleza  kuwa  ni "mzingiro" usio wa haki.

Saudi Arabia , Umoja wa Falme za Kiarabu , Bahrain na  Misri zilivunja  uhusuiano  na  kuiwekea  vikwazo  Qatar  mwezi  uliopita , wakiishutumu kwa  kufadhili  makundi  ya  itikadi  kali  na  kuunga mkono  ugaidi, ambapo mfalme  huyo  anakana.

Katar nach dem Boykott (picture-alliance/AP Photo/Doha News)

Shughuli za manunuzi katika maduka mjini Doha

"Qatar  inapambana  na  ugaidi  bila  kuchoka  na  bila kujali ni  nani, na  jumuiya  ya  kimataifa  inatambua  hilo,"Sheikh Tamim amesema katika  hotuba  yake katika  televisheni.

Amezungumza  masaa  kadhaa  baada  ya  waziri  wa  mambo  ya kigeni  wa  Marekani  Rex Tillerson  amesema  Marekani  inaridhika na  juhudi  za  Qatar  kutekeleza  makubaliano  yenye  lengo  la kupambana  dhidi ya ufadhili  kwa  magaidi, na kuyataka  mataifa hayo  manne  kuondoa  hali ya 2kuizingira nchi hiyo".

Pia  inakuja  siku chache  kabla  ya  rais  wa  Uturuki Recep Tayyip erdogan , ambaye  anaiunga  mkono  Qatar  katika  mzozo  huu, alitaajiwa  kufanya  ziara  nchini  Qatar, Saudi Arabia  na  Kuwait kujaribu  kutatua  mzozo  huo.

Rex Tillerson in Katar (picture-alliance)

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Rex Tillerson akiwa nchini Qatar

Mapema  mwezi  huu wakati  wa   duru  ya  mchakato  wa  kufanya mazungumzo  ya  kidiplomasia,  Tillerson  alitia  saini  makubaliano na  Qatar  kupambana  na dhidi  ya  ufadhili  kwa  makundi  ya kigaidi, sehemu  ya  juhudi  zinazoongozwa na  Kuwait  kujaribu kutatua  tofauti  kubwa  katika  mataifa  washirika  wakubwa  wa mataifa  ya  magharibi  katika  miongo  kadhaa.

Tamko rasmi  kutoka  kwa  mataifa  manne  ya  Kiarabu  bado halijatolewa, lakini  mshauri wa   mfalme  wa  Saudi Arabia amelielezea  kuwa  ni  tamko  lililoandikwa  kama  na  mwanafunzi. "Iwapo lingeandikwa na  mwanafunzi  katika  shule  ya  msingi  basi angekuwa  amebahatisha tu," Saud al-Qahtani ameandika  katika ukurasa  wake wa  Twitter.

Wachambuzi  ambao  wamekaribishwa  na  televisheni  inayomilikiwa na  Saudia  ya  al-Arabiya  pia  imeshutumu  hotuba  hiyo.

"Hii  ni hotuba ya kutojihusisha  ambayo  inatuma  ujumbe kwamba Qatar haitasitisha  kuunga  mkono ugaidi," amesema  Ali al-naimi, mhariri  wa  tovuti  ya  habari  ya  mtandaoni  iliyochapishwa  katika Umoja  wa  falme za  Kiarabu.

Mzozo  huu  unazunguka  katika  madai  kwamba  Qatar  inaunga mkono  makundi  ya  wanamgambo  wa  Kiislamu, ikiwa  ni  pamoja na  Syria na  Libya , na  inawakumbatia  wanachama  wa  kundi  la Udugu  wa  Kiislamu.

Emir Tamim von Qatar und Erdogan (Picture alliance/dpa/Turkish President Press Office)

Mfalme wa Qatar (kushoto) akisalimiana na rais wa Uturuki Erdogan(kulia)

Ilianzia  baada  ya  hotuba mwishoni  mwa  mwezi  Mei iliyotolewa na  Sheikh Tamim  kuonekana  katika  tovuti ya  shirika  la  habari  la taifa , ambalo Doha  inasema  hakuwahi  kuitoa  na  kusema  tovuti hiyo  ilidukuliwa  kutoka  moja  kati  ya  nchi  jirani, ikiinyoshea  kidole Umoja  wa  Falme  za  Kiarabu.

Gazeti  la  Washington Post, likinukuu maafisa  wa  ujasusi , liliripoti wiki  iliyopita  kwamba  Umoja  wa  Falme  za  Kiarabu  ulipanga kudukua mitandao  ya  kijamii  ya  serikali  ya  Qatar na tovuti  za habari  ili  kuweka nukuu bandia. Umoja  wa  Falme za  Kiarabu unakana  kata kata  kuhusika  na  suala  hilo.

Sheikh Tamim  amevieleza  vikwazo  hivyo  kuwa  ni  kampeni ambayo  ilikuwa  inapangwa  dhidi  ya  Qatar , akiita  hatua  ya uchokozi dhidi  ya  sera  za  mambo  ya  kigeni  za  nchi  hiyo.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre

Mhariri: Sudi Mnette

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com