Putin : Crimea ni ya Urusi | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.03.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Putin : Crimea ni ya Urusi

Rais Vladimir Putin wa Urusi Jumanne(18.03.2014)amechukuwa hatua za mwanzo za kulijumuisha jimbo la Ukraine la Crimea Urusi na kuadhimisha uchoraji upya wa mipaka ya Ulaya tokea kumalizika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Rais Vladimir Putin wa Urusi.

Rais Vladimir Putin wa Urusi.

Putin hapo amelitaarifu rasmi bunge juu ya ombi la Crimea kujiunga na Urusi na kuzielekeza taasisi za taifa kuidhinisha makubaliano ya kuifanya Crimea kuwa sehemu ya nchi hiyo.

Putin anatazamiwa kuhutubia mabaraza yote ya bunge mchana huu baada ya hapo jana kuutambuwa uhuru wa Crimea kwa kile kinachoonekana kuwa hatua ya mwanzo ya kuifanya iwe ardhi iliomo ndani ya mipaka ya Urusi.

Kunyakuliwa kwa jimbo la Crimea na vikosi vyenye kuunga mkono Urusi kufuatia kuangushwa kwa rais wa Ukraine anayeungwa mkono na Urusi, Viktor Yanukovych, mwezi uliopita kumelaaniwa duniani kote na Marekani na Umoja wa Ulaya hapo jana zimetangaza vikwazo vya kwanza dhidi ya baadhi ya maafisa wa serikali ya Urusi.

Unyakuzi wa Crimea walaaniwa

Shamra shamra za kusheherekea matokeo ya kura ya maoni katika mji mkuu wa Crimea,Simferopo. (16.03.2014)

Shamra shamra za kusheherekea matokeo ya kura ya maoni katika mji mkuu wa Crimea,Simferopo. (16.03.2014)

Lakini vikwazo hivi havitazamiwi kumzuwiya Putin anayezidi kuwa mkaidi ambaye ameazimia kuhalalisha unyakuaji wa Crimea kutokana na kura ya maoni ya mwishoni wa juma lililopita kwenye jimbo hilo ambapo takriban asimilia 97 ya wakaazi wake walipiga kura ya kujitenga kutoka Ukraine na kuwa sehemu ya Urusi.

Sergei Naryshkin spika wa bunge la taifa nchini Urusi la Duma amesema rais atauelezea msimamo wake kuhusiana na ombi la Crimea kuwa sehemu ya Urusi kwa kuzingatia matokeo ya kura ya maoni.

Kutokana na kuwepo kwa uungaji mkono mkubwa wa hatua hiyo ndani ya Urusi kwenyewe maelfu ya watu wanatazamiwa kuandamana leo hii katikati ya Moscow kwa kauli mbiu "Tuko Pamoja" baada ya hotuba ya Putin.

Rasi hiyo iliostawi imekuwa kambi ya vikosi vya majini vya Urusi tokea mwishoni mwa karne ya 18 na imekuja tu kuwa sehemu ya Ukraine hapo mwaka 1954 baada ya kiongozi wa Muungano wa Kisovieti Nikita Khrushchev kuihamisha kutoka Urusi.

Vikwazo kutoiyumbisha Urusi

Rais Barack Obama wa Marekani akitangaza vikwazo dhidi ya maafisa wa Urusi na Ukraine mjini Washington. ( 17.03. 2014)

Rais Barack Obama wa Marekani akitangaza vikwazo dhidi ya maafisa wa Urusi na Ukraine mjini Washington. ( 17.03. 2014)

Kuzuiliwa kwa mali na marufuku ya safari kulikotangazwa na Marekani na Umoja wa Ulaya ambako kunaonekana kuwa ni vikwazo vikubwa kuwahi kuwekwa dhidi ya Urusi tokea kumalizika kwa Vita Baridi inaonekana kutotosha kuishawishi Urusi kubadili mawazo.

Lakini suala kubwa linaloendelea kubakia ni iwapo Urusi baada ya hatua hiyo ya kuinyakua Crimea itakuwa imefikia kikomo cha njozi yake au iwapo bado itaendelea kuyamezea mate majimbo mengine yenye idadi kubwa ya watu wenye kuzungumza Kirusi ya kusini na mashariki ya Ukraine.

Vikwazo vililvyowekwa na Rais Obama wa Marekani kwa maafisa 11 wa Urusi na Ukraine akiwemo Rais wa zamani wa Ukraine Viktor Yanukovich na washauri wawili wa Rais Putin lakini Putin mwenye hayumo kwenye orodha hiyo ya kuwekewa vikwazo.

Licha ya kulaani vikali kwa kura ya maoni ya Crimea,mataifa ya magharibi yamekuwa na tahadhari katika kuchukuwa hatua za kwanza dhidi ya Urusi kwa nia ya kuacha mlango wazi wa kufikia ufumbuzi wa mzozo huo kwa njia ya kidiplomasia.

Mwandishi: Mohamed Dahman /AFP/ Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com