1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Poroshenko asema Ukraine iko tayari

Admin.WagnerD19 Agosti 2016

Rais wa Urusi Vladimir Putin amewasili katika jimbo la Krimea lililokuwa sehemu ya Ukraine. Ziara yake inakuja siku chache baada ya kuilaumu Ukraine kwa kujaribu kuivamia sehemu hiyo

https://p.dw.com/p/1Jltn
Rais Vladimir Putin akiongoza mkutano wa baraza la usalama
Rais Vladimir Putin akiongoza mkutano wa baraza la usalamaPicha: Reuters/A. Druzhinin

Rais Putin anatarajiwa kuongoza mkutano wa baraza lake la usalama unaofanyika katika jimbo hilo la Krimea na pia atakutana na vijana. Hii ni mara ya sita kwa Rais huyo kufanya ziara katika sehemu hiyo tangu Urusi ilipoiteka mnamo mwezi wa Machi 2014.

Wiki iliyopita Putin aliishutumu Ukraine kwa alichoita vitendo vya kigaidi kwa kuingiza makundi ya kufanya hujuma baada ya mkasa uliotokea kwenye mpaka baina ya Ukraine na Krimea.

Maafisa wawili wa kijeshi wa Urusi waliuliwa katika kadhia hiyo.Hata hivyo Ukraine imekanusha kuhusika na mauaji ya maafisa hao.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko alisema hapo jana kwamba pana uwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa mvutano na Urusi na amesema hawezi kuondoa uwezekano wa Urusi kufanya uvamivi kamili kwenye pande zote.

Lakini Poroshenko ametamka kwamba nchi yake iko tayari.Amesema uwezekano wa kuzuka mapigano ni mkubwa sana. Ameeleza kuwa hawezi kuweka kando uwezekano wa Urusi kufanya uvamizi katika pande zote.

Lakini amesema majeshi ya Ukraine yapo tayari kumkabili adui katika upande wa mashariki ambako adui analikalia jimbo la Donbass na pia kwenye mpaka na Crimea.Rais Poroshenko amesema ikiwa hali itazidi kuwa mbaya maandalizi ya kijeshi yatafanyika na hali ya hatari itatangazwa ambapo sheria za kijeshi zitatumika.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko
Rais wa Ukraine Petro PoroshenkoPicha: Reuters/J. Dudek

Putin ataka Ukraine iwe na busara

Rais Putin amesema anatumai Ukraine itazingatia busara katika mgogoro wa kidiplomasia. Putin ametamka kwamba Urusi haitavunja uhusiano wa kibalozi na Ukraine licha ya viongozi wa nchi hiyo kutokuwa tayari kujenga uhusiano kamili wa kidiplomasia.

Rais wa Urusi ameeleza kuwa nchi yake itaendelea kudumisha uwezekano wa mawasiliano na Ukraine.

Lakini Rais Putin pia ameeleza kuwa yeye pamoja na maafisa wake watajadili juu ya hatua nyingine zinazopaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha kwamba jimbo la Crimea linalindwa vizuri zaidi katika siku za usoni.

Wakati huo huo majeshi ya Urusi ya majini na nchi ya kavu yamefanya mazoezi katika jimbo la Crimea. Wizara ya ulinzi ya Urusi imefahamisha kwamba mazoezi ya kijeshi makubwa zaidi yatafanyika mwezi ujao katika jimbo hilo.

Luteka hiyo inafanyika katika muktadha wa kuongezeka kwa mvutano baina ya Urusi na Ukraine. Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema Waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Sergei Shoigu alikuwapo kwenye mazoezi hayo.

Mwandishi:Abdu Mtulya

Mhariri:Josephat Charo