1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaUrusi

Putin aashiria Ukraine imehusika shambulizi la Moscow

23 Machi 2024

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema hatua za ziada za kiusalama zimechukuliwa kote nchini humo, baada ya shambulio la bunduki kwenye jumba moja la starehe mjini Moscow lililosababisha vifo vya watu 133.

https://p.dw.com/p/4e3dt
Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Kremlin.ru/REUTERS

Pia ameashiria kwamba Ukraine huenda imehusika hilo lililowajeruhi mamia wengine. 

Akihutubia taifa baada ya shambulio hilo lililotajwa na viongozi mbalimbali ulimwenguni kuwa la kigaidi, Putin amesema watu wanne ambao wanashukiwa kuhusika moja kwa moja na mkasa huo wamekamatwa wakijaribu kuvuka mpaka ili kuingia Ukraine. Hata hivyo hakutoa ushahidi wowote.

Aidha Putin ameitangaza siku ya Jumapili kuwa ni maombolezo ya kitaifa. Baadhi ya Wabunge wa Urusi pia waliinyooshea kidole Ukraine kuhusika na shambulio hilo, hatua ambayo imekanushwa vikali na mshauri wa rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, Mykhailo Podolyak akisema utawala mjini Kyiv haujawahi kutumia njia za "kigaidi."