1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Papa yupo ziarani Guinea ya Ikweta, ziara ya mwisho Afrika

21 Aprili 2026

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Leo XIV anaanza awamu ya mwisho ya ziara yake barani Afrika katika nchi ya Guinea ya Ikweta.

https://p.dw.com/p/5CaDy
Kamerun Yaoundé 2026 | Papst Leo XIV
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Leo XIVPicha: Vatican Media/Catholic Press Photo/ipa-agency/picture alliance

Papa anatarajiwa kupaza sauti zaidi katika kutetea haki za binadamu, kwenye nchi hiyo ambayo ni miongoni mwa baadhi ya nchi za barani Afrika, zinazokandamiza vyombo vya habari, upatikanaji wa intaneti na uhuru wa kujieleza.

Baada ya ziara ya siku tatu nchini Angola, Papa Leo anatarajiwa kuwasili katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati, inayotawaliwa tangu mwaka 1979 na Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, mwenye umri wa 83. Ni Rais aliyemo madarakani kwa muda mrefu zaidi duniani.

Papa Leo amepangiwa baadae kuzungumza na Rais Nguema, viongozi wa serikali, wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa asasi za kiraia na wale wa sekta ya utamaduni.

Kesho Jumatano, ataongoza Misa kwenye ngome ya Obiang Mongomo na kisha atwatembelea wanafunzi na walimu katika shule ya teknolojia iliyopewa jina la  Papa Francis.

Kisha atazuru mji mkuu wa kiuchumi wa Bata kutoa heshima kwa waathiriwa wa mlipuko wa mwaka 2021, uliosababisha vifo vya zaidi ya watu 108, katika kambi ya kijeshi na pia Atawatembelea wafungwa katika gereza la Bata.

Siku ya Alhamisi, Papa Leo ataongoza Misa kubwa katika uwanja wa Malabo kabla ya kukamilisha safari yake ya siku 10 katika miji na vijiji 11 kwenye nchi nne za Afrika.